Wakimbizi wa kambi ya Dadaab Kenya waanza kurejeshwa makwao
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i10435-wakimbizi_wa_kambi_ya_dadaab_kenya_waanza_kurejeshwa_makwao
Oparesheni ya kuwarejeshwa makwao wakimbizi waliokuwepo katika kambi ya Dadaab huko Kenya imeanza licha ya kuwepo juhudi za kimataifa za kutaka kuzuia zoezi hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 02, 2016 07:52 UTC
  • Wakimbizi wa kambi ya Dadaab Kenya waanza kurejeshwa makwao

Oparesheni ya kuwarejeshwa makwao wakimbizi waliokuwepo katika kambi ya Dadaab huko Kenya imeanza licha ya kuwepo juhudi za kimataifa za kutaka kuzuia zoezi hilo.

Duru za habari zimearifu kuwa, kundi la kwanza la wakimbizi wa kambi hiyo ambao wengi wao ni raia wa Somalia walirejeshwa nyumbani jana Ijumaa. Wakimbizi wa Kisomali waliikimbia nchi yao baada ya kuanza vita vya ndani, ukame, baa la njaa na mashambulizi ya kigaidi yanayoendelea kwa kipindi cha miaka 25 iliyopita na kuelekea katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab huko mashariki mwa Kenya. Mbali na raia wa Somalia, wakimbizi wengine kutoka nchi jorani wakiwemo wakimbizi kutoka Uganda, Eritrea, Sudan Kusini na Ethiopia pia wanaishi kwenye kambi hiyo kubwa zaidi duniani.

Awali kambi ya Dadaab ilikuwa imepangiwa kutoa hifadhi kwa wakimbizi elfu tisini tu. Hata hivyo ripoti ya wasimamizi inaeleza kuwa, kwa sasa zaidi ya wakimbizi laki tano wanaishi kwenye kambi hiyo.

Miezi kadhaa iliyopita maafisa wa Kenya walitangaza kuwa, wana mpango wa kuifunga kambi ya Dadaab. Kambi hiyo inatazamiwa kufungwa kikamilifu kabla ya mwezi Mei mwaka 2017. Hata hivyo uamuzi huo na Kenya umekabiliwa na upinzani mkubwa huku viongozi mbalimbali wa nchi za eneo hilo na taasisi za kimataifa wakiitaka serikali ya Kenya kutupilia mbali uamuzi huo. Viongozi hao wanasema uamuzi huo wa Kenya wa kuifunga kambi ya wakimbizi ya Dadaab ni kinyume na sheria za kimataifa.

Pamoja na hayo yote, Kenya inaendelea kutilia mkazo uamuzi wa kufungwa kambi hiyo na tayari imeanzisha mchakato wa kuifunga baada ya kuundwa kamati ya pande tatu ya kushughulikia suala hilo.

Kamati ya pande tatu ya kufuatilia zoezi la kuwarejesha makwao wakimbizi wa Dadaab imetangaza kuwa nusu uya wakimbizi waliokuwa wakiishi katika kambi ya Dadaab watakuwa wamerejeshwa katika nchi zao hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

Wakati huo huo Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) linasisitiza kwamba serikali ya Kenya inapasa kujiepusha na hatua yoyote inayokiuka sheria za kimataifa za kuwalinda raia wanaohitajia msaada.

Viongozi wa Kenya wamesema kuwa wanaifunga kambi ya Dadaab kutokana na wasiwasi wa kiuchumi, mazingira na masuala ya kiusalama. Viongozi hao walisema kuwa matatizo ya kiuchumi na gharama kubwa za kusimamia kambi hiyo haziruhusu kuendelea kuishi wakimbizi katika kambi hiyo.

Wakati huo huo weledi wa mambo wanasema kuwa kujitokeza hofu ya kuwepo magaidi na kuongezeka hujuma za ugaidi katika eneo hilo ni moja kati ya sababu kuu za kufungwa kambi ya Dadaab. Kenya ni miongoni mwa nchi ambazo zimeathiriwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya kundi la kigaidi la wanamgambo wa al Shabab lenye makao yake huko Somalia.

Wanafunzi 140 wa Chuo Kikuu cha Garisa huko Kenya waliuawa katika mashambulizi yaliyofanywa na magaidi wa al Shabab chuoni hapo mwaka uliopita. Baadhi ya viongozi wa Kenya wanasema kuwa makundi ya kigaidi yanajipenyeza katika kambi za wakimbizi na kupanga mashambulizi ya kigaidi katika kambi hizo.

Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa kufungwa kambi ya wakimbizi ya Dadaab kutaandaa fursa nzuri zaidi kwa makundi ya kigaidi kuweza kuwasajili wanamgambo wapya kwa ajili ya kujiunga na makundi hayo. Wanasema kuwa wakimbizi wengi wataendelea kukabiliwa na matatizo ya kiuchumi na kiusalama wakati wakirejea makwao na ka msingi huo yumkini wakashawishiwa na makundi mengi ya kigaidi kwa ahadi za kuwapa ahadi za hali bora ya kiuchumi na kuwadhaminia usalama.

Weledi wa mambo wanasema kuwa si Somalia pekee, bali aghalabu ya nchi za eneo hilo la Afrika zinakabiliwa na vita, ukame na harakati za makundi ya kigaidi; kwa msingi huo kufungwa kambi ya wakimbizi ya Dadaab si tu kwamba ni kitendo kisicho cha kibinadamu, bali hatua hiyo itasababisha mgogoro wa muda mrefu katika eneo hilo.