Nov 21, 2023 07:59 UTC
  • Joseph Boakai atangazwa mshindi wa uchaguzi wa rais wa Liberia

Mwanasiasa mkongwe Joseph Boakai jana Jumatatu alitangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa rais wa Liberia, akimshinda George Weah aliyebwagwa katika duru ya pili ya uchaguzi huo. Haya ni kwa mujibu wa tangazo la Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Liberia (NEC) baada ya kukamilisha zoezi la kuhesabu kura.

Davidetta Browne Lansanah Mkuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Liberia ameeleza kuwa  Boakai ameshinda kwa asilimia 50.64 ya kura, dhidi ya asilimia 49.36 ya kura za mpinzani wake nyota wa zamani wa kimataifa George Weah. Boakai ameibuka mshindi akimpita Weah kwa kura 20,567 pekee. 

Ijumaa iliyopita  George Weah alikiri  kushindwa na mpinzani wake Boakkai katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais kwa mujibu wa matokeo ya kura yaliyotangazwa ya zaidi asilimia 99.98 za kura zilizokuwa zimekwishahesabiwa.  

George Weah

Rais huyo wa Liberia anayeondoka madarakani na nyota wa zamani wa kandanda jana alisifiwa na kupongezwa na shakhsia mbalimbaili kutoka nje ya nchi kwa hatua yake ya kukubali matokeo hayo ya uchaguzi wa rais na hivyo kutoa fursa ya kukabidhi madaraka kwa rais mpya kwa njia ya amani. 

Kufuatia matokeo hayo ya uchaguzi wa rais wa Liberia, Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (Ecowas) pia imetoa taarifa na kusema: Wananchi wa Liberia kwa mara nyingine tena wamedhihirisha kuwa demokrasia iko hai katika ukanda wa Ecowas na kwamba mabadiliko yanawezekana kupitia njia za amani." 

 

Tags