Dec 01, 2023 06:47 UTC
  • Mama wa miaka 70 Uganda awa mwanamke mkongwe zaidi kujifungua Afrika

Ajuza wa miaka 70 huko nchini Uganda ameingia katika madaftari ya kumbukumbu kwa kuwa mwanamke wa kwanza mwenye umri mkubwa kujifungua barani Afrika.

Safina Namukwaya alijifungua pacha Jumatano kwa njia ya upasuaji katika hospitali moja mjini Kampala. Madaktari katika hospitali hiyo wanasema mzazi huyo na wanawe wanaendelea vizuri.

Habari zaidi zinasema kuwa, Namukwaya alipata ujauzito kupitia njia ya kitaalamu ya In Vitro Fertilization (IVF). Pacha hao wamezaliwa baada ya wiki 34, na wote walikuwa na uzani wa takriban kilo 2 wakati wa kuzaliwa.

Kwa mujibu wa taasisi ya afya alikojifungulia ya Women's Hospital International and Fertility Centre mjini Kampala, Namukwaya ameweka historia kwa kuwa mwanamke mkongwe zaidi kujifungua barani Afrika.

Taarifa ya hospitali hiyo imesema: Tunapoadhimisha miaka 20, tumefanikiwa kumzalisha mwanamke mkongwe zaidi barani Afrika. Mama wa pacha mwenye miaka 70.

Mwanamke huyo ameiambia kanali ya NTV ya Uganda kuwa, alipitia kipindi kigumu wakati wa ujauzito, ikiwemo kutelekezwa na mumewe.

"Wanaume wanaogopa kuwa baba wa watoto pacha, mume wangu hajawahi kukanyaga katika hospitali hii tangu nilipolazwa," amesema Namukwaya.

Halima Cisse, mama aliyejifungua watoto 9 miaka 3 iliyopita

Si vibaya kukumbusha hapa kuwa, mwaka 2021 katika tukio jingine la aina yake, mwanamke mmoja raia wa Mali alijifungua watoto tisa kwa mpigo katika hali ambayo sio ya kawaida.

Halima Cisse, wakati huo akiwa na umri wa miaka 25, alijifungua watoto wa kike watano na wavulana wanne katika hospitali moja nchini Morocco.

Tags