Njaa yaua watu 176 eneo la Tigray, Ethiopia
Watu wasiopungua 176 wameaga dunia katika eneo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia kutokana na njaa iliyosababishwa na ukame ambao umeendelea kushuhudiwa katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo.
Mshirikishi wa Eneo, Hadush Asemelash aliiambia kanali ya Tigray TV jana Jumatano kuwa, wanawake 75 ni miongoni mwa watu waliopoteza maisha kutokana na njaa katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Anadolu, watu 24 wameaga dunia katika Wilaya ya Tsaeda Emba jimboni Tigray, na ndio wahanga wa hivi karibuni wa makali ya njaa katika eneo hilo.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, zaidi ya watu 50 waliripotiwa kuaga dunia katika maeneo ya kaskazini mwa Tigray na Amhara huko nchini Ethiopia kutokana na njaa.
Hivi karibuni, Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Ethiopia (EHRC) ilisema wakimbizi zaidi ya 30 wamepoteza maisha kutokana na njaa na utapiamlo katika jimbo la Gambella lililoko magharibi ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Kwa ujumla, watu zaidi ya 200 wamepoteza maisha katika wiki za hivi karibuni kutokana na njaa iliyosababishwa na ukame ambao umeendelea kushuhudiwa katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo.
Huku maeneo ya kaskazini mwa Ethiopia yakikabiliwa na ukame mkubwa, baadhi ya maeneo ya kusini na mashariki mwa nchi hiyo yamekumbwa na mvua kubwa za el-Nino.
Pembe ya Afrika na eneo zima la Mashariki mwa Afrika linakabiliwa na mabadiliko makubwa ya hali ya hewa ya el-Nino, kuanzia hali ya ukame na kukumbwa na mafuriko, masuala yanayosababisha maafa kwa jamii.