Wanachuo wa Kiislamu wa Uganda watakiwa kuwa na umoja
Kongamano la Wanafunzi wa Vyuo Vikuu nchini Uganda lililosimamiwa na ofisi ya Utamaduni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lilimaliza kazi zake jana mjini Kampaka kwa kusisitiza udharura wa kuimarishwa umoja baina ya Waislamu.
Mwambata wa utamaduni wa Iran nchini Uganda, Ali Bakhtiyari alisema katika sherehe za kuhitimisha kongamano hilo kwamba kuna udharura wa kutiliwa maanani zaidi mafundisho ya Uislamu na matatizo na changamoto mbalimbali zinazowakabili wafuasi wa dini hiyo.
Bakhtiyari amesema kuwa, kongamano hilo ni fursa ya kuonesha kivitendo umoja na mshikamano wa Kiislamu.
Mwambata wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Uganda amesema matatizo mengi yanayousumbua ulimwengu wa Kiislamu na jamii zisizo za Kiislamu ni kutoijua dini na mafundisho yake.
Kongamano la Wanachuo Waislamu nchini Uganda ambalo limehudhuriwa na wanafunzi 500 wa vyuo vikuu nchini humo limefanyika kwa muda wa siku tatu. Kongamano hilo pia lilijumuisha mashindano ya Qur'ani tukufu na mafundisho ya Uislamu.