Uganda: Kizza Besigye apinga kuwekwa kizuizini katika kesi ya uhaini inayomkabili
-
Kizza Besigye
Kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Kizza Besigye, amewasilisha ombi mahakamani akitaka kutolewe uamuzi wa kusimamisha kuendelea kushikiliwa kizuizini na kufunguliwa mashtaka.
Besigye ambaye amekuwa kizuizini tangu alipotekwa nyara Nairobi nchini Kenya Novemba mwaka 2024, amesema kuwa serikali ya Uganda imekiuka haki zake.
Katika maombi yake kwa Mahakama Kuu, Besigye amemtaja Muhoozi Kainerugaba, Mkuu wa Jeshi la Uganda na mtoto wa Rais wa nchi hiyo Yoweri Museveni kuwa anahusika na ombi lake hilo.
Kainerugaba mwaka jana alituma ujumbe katika akaunti yake ya X ambapo alitishia kumnyonga kiongozi huyo wa upinzani kutokana na kile alichokiita " Jaribio la kutaka kumuuwa baba yake."
Besigye na msaidizi wake wameshtakiwa kwa uhaini huku kesi hiyo ikitarajiwa kuanza Alhamisi wiki hii. Mashirika ya kutetea haki za binadamu na wapinzani nchini Uganda wameeleza kuwa mashtaka hayo yamechochewa kisiasa.
Besigye, daktari wa zamani wa Rais wa Uganda Yoweri Museveni na mpinzani wake wa kisiasa kwa zaidi ya miaka 25, amekuwa akifungwa na kutoka jela tangu alipoibua upinzani dhidi ya Museveni kwa mara ya kwanza mwaka 2001.