Mapigano ya kikabila yameua zaidi ya 15,000 katika mji mmoja Sudan
(last modified Sat, 20 Jan 2024 07:21:17 GMT )
Jan 20, 2024 07:21 UTC
  • Mapigano ya kikabila yameua zaidi ya 15,000 katika mji mmoja Sudan

Ripoti ya Umoja wa Mataifa imesema watu kati ya 10,000 na 15,000 waliuawa katika ghasia na mapigano ya kikabila mwaka jana katika mji mmoja ulioko katika jimbo la Darfur Magharibi nchini Sudan.

Shirika la habari la Reuters limeripoti habari hiyo na kueleza kuwa, kati ya Aprili na Juni mwaka jana 2023, mji wa el-Geneina ulishuhudia mapigano makali ya kikabila yaliyosababisha vifo vya maelfu ya watu.

Duru mbalimbali zinavituhumu Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) na wanamgambo waitifaki wake wa Kiarabu kuhusika na mashambulizi hayo ambayo wadadisi wa mambo wanasema yanaweza kuwa jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu. Umoja wa Mataifa umeonya pia juu ya uwezekano wa kushuhudiwa jinai dhidi ya binadamu huko Darfur na kutahadharisha kuwa mzozo unaoendelea jimboni humo umechukua mwelekeo wa kikabila katika eneo hilo.

Wakati huo huo, idadi ya watu wanaokimbia machafuko katika jimbo la Darfur huko Sudan inaripotiwa kuongezeka kufuatia wimbi jipya la mauaji ya kikabila. Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya UN, baina ya Juni 14 na 17, watu zaidi ya 12,000 waliukimbia mji wa el-Geneina kwa miguu na kuingia nchini Chad kupitia mji wa Adre, wakihofiwa kuuawa.

Makaburi ya umati jimboni Darfur

Haya yanajiri huku Umoja wa Mataifa ukisema kuwa, zaidi ya watu 12,000 wameshauawa na zaidi ya milioni 7.4 wamekimbia makazi yao ndani na nje ya Sudan tangu mapigano baina ya Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF na Jeshi la Sudan SAF kwa ajili ya kuhodhi madaraka ya nchi yalipozuka huko Sudan Aprili mwaka jana.

Hadi sasa juhudi za upatanishi za kieneo na kimataifa za kuhitimisha mapigano hayo na kuzishawishi pande hasimu kuketi kwenye meza ya mazungumzo zimegonga mwamba. Hata hivyo siku chache zilizopita, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) Moussa Faki Mahamat aliwateua watu watatu mashuhuri wa Kiafrika kuwa wajumbe wa jopo la ngazi ya juu la AU la kushughulikia mgogoro wa Sudan.