Feb 14, 2024 07:35 UTC
  • Jeshi la Ethiopia latuhumiwa kuua makumi ya raia jimboni Amhara

Kamisheni ya Haki za Kibinadamu ya Ethiopia (EHRC) imedai kuwa wanajeshi wa serikali ya Ethiopia waliwaua raia wasiopungua 45 wa mji wa Merawi katika jimbo la Amhara la kaskazini mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Taarifa ya jana Jumanne ya taasisi hiyo ya kiraia imesema, maafisa usalama wa Serikali ya Federali ya Ethiopia mnamo Januari 29 waliwaua kwa kuwapiga risasi kinyume cha sheria wakazi 45 wa Merawi, kwa tuhuma za kuwaunga mkono wanamgambo wa Harakati ya Kitaifa ya Amhara FANO.

EHRC pia imeeleza kwamba, mnamo Januari 19, kwa akali watu 15, wakiwemo wanawake waliuawa katika eneo la Yeidwuha, yapata kilomita 160 kusini mwa Bahir Dar, wakati wa msako wa nyumba zilizoko karibu na eneo la mapigano.

Mapema mwezi huu, Bunge la Ethiopia lilirefusha muda wa hali ya hatari iliyotangazwa Agosti mwaka uliopita 2023 katika eneo hilo linaloshuhudia mapigano la Amhara, kwa kipindi cha miezi minne.

Wanamgambo katika jimbo la Amhara

Eneo la Amhara nchini Ethiopia limeripotiwa kuendelea kushuhudia mapigano makali kati ya wanajeshi wa serikali ya shirikisho na wanamgambo wa eneo hilo. Ghasia hizo huko Amhara, ambalo ndilo eneo la karibuni zaidi lililozuka machafuko nchini Ethiopia, zilisababisha kutangazwa hali ya hatari mwezi Agosti mwaka jana.

Umoja wa Afrika mara kadhaa umeitaka serikali ya Ethiopia kufanya mazungumzo na wanamgambo katika eneo la Amhara ili kupata suluhisho la amani.

Mapigano hayo makali yalizuka tangu Julai 2023 kati ya Jeshi la Ethiopia (ENDF) na wanamgambo wa Harakati ya Kitaifa ya Amhara FANO juu ya uamuzi wa serikali wa kuunganisha vikosi vya kikanda katika polisi ya shirikisho au jeshi.

Tags