Iran, Ethiopia zajadili BRICS, uhusiano wao na masuala ya kieneo
(last modified Wed, 23 Oct 2024 10:24:54 GMT )
Oct 23, 2024 10:24 UTC
  • Iran, Ethiopia zajadili BRICS, uhusiano wao na masuala ya kieneo

Katika mkutano muhimu wa kidiplomasia, Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian amekutana na Abiy Ahmed, Waziri Mkuu wa Ethiopia, ambapo wamejadili masuala muhimu ya pande mbili na kikanda.

Pezeshkian ameeleza kuwa, kuingia kwake katika kinyang'anyiro cha urais kulichochewa na nia ya kuwepo kwa uwiano wa kijamii ndani ya Iran na uhusiano mkubwa wa kimataifa; masuala ambayo yaliugusa umma wa Wairani.

Kadhalika Dakta Pezeshkian amelaani vikali jinai na mienendo ya utawala wa Israel na kusema kwamba, hatua za utawala huo ikiwa ni pamoja na mauaji ya shakhsia mashuhuri wa Palestina katika siku ya kwanza ya uongozi wake, zilivuruga juhudi za Iran za kutafuta amani.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika wakati wa ziara ya Pezeshkian nchini Russia, Rais wa Iran amesisitiza umuhimu wa kundi la BRICS katika kurekebisha mifumo isiyo ya haki ya kimataifa na kikanda.

Mkutano wa viongozi wa BRICS umeanza rasmi leo na utamalizika kesho Okt 24

Aidha Rais wa Iran amesema anatumai kuwa, uhusiano na ushirikiano wa pande mbili wa Jamhuri ya Kiislamu na Ethiopia katika nyuga mbali mbali utaboreka na kuimarika zaidi.  Vile vile amekosoa uungaji mkono wa Magharibi kwa Israel, akisisitiza kwamba vitendo vyovyote vya uhasama vya Wazayuni dhidi ya Iran vitalilazimisha taifa hili lijibu mapigo kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed sanjari na kukiri uwepo wa sifa na haiba nzuri ya Iran nchini Ethiopia na kuelezea wasiwasi wake juu ya matukio yanayojiri katika eneo amesema kwamba, Iran ni taifa lenye nguvu na huru. Amegusia juu ya kukosekana kwa usawa katika miundo ya kimataifa na kikanda huku akisisitiza kwamba, taasisi kama BRICS zina jukumu muhimu katika kushughulikia tofauti zilizopo.

Tags