Feb 24, 2024 02:14 UTC
  • UN: Makumi ya watu wamebakwa, kunyanyaswa kingono nchini Sudan

Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema katika ripoti yake mpya iliyotolewa jana Ijumaa kwamba makumi ya watu, wakiwemo watoto, wamekuwa waathiriwa wa ubakaji na aina nyingine za unyanyasaji wa kingono katika mzozo unaoendelea nchini Sudan, vitendo ambavyo vinaweza kutambuliwa kuwa ni uhalifu wa kivita.

Ripoti hiyo ambayo inahusu kipindi cha kuanzia mwanzoni mwa mapigano ya ndani ya Sudan hadi Desemba 15, imesajili unyanyasaji unaofanyika katika nchi ambayo kwa kiasi kikubwa imekuwa vigumu kwa mashirika ya misaada na waangalizi wa haki za binadamu kufikia huko, suala ambalo linaficha athari mbaya za mzozo huo ambao umegubikwa na vita katika maeneo mengine ya dunia kama vile mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel katika Ukanda Gaza na vita vya Ukraine.

Ripoti hiyo inasema kuwa, takriban watu 118 walikuwa waathiriwa wa ukatili wa kijinsia, ikiwa ni pamoja na ubakaji, na kwamba mashambulizi mengi yalifanywa na askari, majumbani na mitaani.

Ripoti hiyo imetoa mfano wa mwanamke mmoja wa Sudan ambaye "alizuiliwa katika jengo moja na kubakwa na genge la watu kwa siku 35" .

Wakimbizi Sudan

Ripoti hiyo pia inaangazia kadhia ya kuajiri watoto kama askari vitani kunakofanywa na pande zote mbili zinazozozana nchini Sudan.

Volker Türk, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema: "Baadhi ya ukiukwaji huu unaweza kutambuliwa kuwa uhalifu wa kivita," na ametoa wito wa kufanyika uchunguzi wa haraka, wa kina na huru kuhusu madai ya unyanyasaji na ukiukaji wa haki za binadamu nchini Sudan.

Ripoti hiyo imetegemea mahojiano na wahanga na mashahidi zaidi ya 300, baadhi yao yalifanyika Ethiopia na Chad, nchi jirani ambako Wasudani wengi wamekimbilia, pamoja na uchambuzi wa picha, video na picha za satalaiti zilizopigwa katika maeneo yenye migogoro.

Tags