Mar 06, 2024 11:42 UTC
  • Karibu laki 1 wakimbia makwao kutoka na hujuma za wanamgambo Msumbiji

Makumi ya maelfu ya raia wamelazimika kuyakimbia makazi yao nchini Msumbiji baada ya kuibuka tena machafuko kaskazini mwa nchi hiyo.

Hayo yalisemwa jana Jumanne na shirika la kutetea haki za binadamu la Save the Children na kuongeza kuwa, makabiliano baina ya magenge ya wanamgambo na maafisa usalama yamesababishwa watu 99,313, wakiwemo watoto 61,492  kuyakimbia makazi yao katika mkoa wa kaskazini wa Cabo Delgado.

Save the Children imeeleza kuwa, ghasia hizo zimesababishwa idadi hiyo kubwa ya watu kuyakimbia makazi yao katika wilaya kadhaa mkoani Cabo Delgado baina ya Disemba 22, 2023 na Machi 3, 2024.

Kabla ya hapo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwashughulikia Wakimbizi UNHCR lilisema kuwa, hujuma za makundi ya wanamgambo waliojihami kusini mwa Cabo Delgado, zimepelekea maelfu ya watu aghalabu yao wakiwa ni watoto wadogo kutoroka makazi yao, na kukimbilia mahali salama.

Wanachama wa ISIS nchini Msumbiji

Mashambulizi ya makundi ya kigaidi na kundi la kigaidi la ISIS au Daesh huko Cabo Delgado yameua maelfu ya watu tangu mzozo ulipozuka mwaka wa 2017, na kuvuruga miradi ya mabilioni ya dola ya gesi asilia na uchimbaji madini.

Machi mwaka 2021, magaidi nchini Msumbiji waliuteka mji wa Palma wa kaskazini mwa nchi hiyo ulioko katika mpaka wa nchi hiyo na Tanzania, na kuua makumi ya watu na kuwalazimisha kuwa wakimbizi watu wengine zaidi ya 540,000. Eneo hilo limekumbwa na uasi baada ya kuanza mradi wa gesi wa dola bilioni 20.

Mwezi Julai mwaka 2021 Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika SADC ilianza kutuma wanajeshi wake kulisaidia jeshi la Msumbiji kupambana na magaidi waliojizatiti kaskazini mwa nchi hiyo.

Tags