Mar 18, 2024 05:11 UTC
  • Waziri wa Wanawake Zimbabwe  apongeza ustawi mkubwa wa wanawake wa Iran

Waziri wa Masuala ya Wanawake, Maendeleo ya Jamii, Biashara Ndogo na za Kati wa Zimbabwe Monica Mutsvangwa amesifu maendeleo yaliyofikiwa na wanawake wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na hatua zinazochukuliwa na serikali ya Iran kuwawezesha wanawake nchini.

Mutsvangwa ameyasema hayo katika mkutano na Makamu wa Rais wa Iran anayehusika na masuala ya Wanawake na Familia Datka Ensiyeh Khazali pamebizoni mwa kikao cha 68 cha mwaka cha Tume ya Hali ya Wanawake ya Umoja wa Mataifa kinachofanyika katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York kuanzia Machi 11-22.

Waziri huyo wa Zimbabwe aidha amesema vikwazo vya kiuchumi visivyo vya haki na vya upande mmoja vilivyowekwa na madola ya Magharibi dhidi ya Iran na Zimbabwe vimeongeza mashinikizo dhidi ya wanawake na wasichana katika nchi zote mbili.

Amebainisha matumaini kuwa pande hizo mbili zinaweza kushirikiana katika kuwawezesha wanawake na kuwatengenezea ajira, akisema kuwa serikali ya Zimbabwe inatilia maanani umuhimu wa kuweka mazingira salama kwa wanawake kwa ajili ya kushiriki katika shughuli za kijamii.

Makamu wa rais wa Iran kwa upande wake amesema kuwa nchi hizo mbili zinaweza kushirikiana katika kulinda maadili kama sehemu ya juhudi za kuwalinda wasichana katika kukabiliana na vitisho vinavyotokana na mahusiano ya kijamii.

Makamu wa Rais wa Iran anayehusika na masuala ya Wanawake na Familia Datka Ensiyeh Khazali  (kushoto) akiwa na Waziri wa Masuala ya Wanawake wa Nigeria Uju Kennedy Ohanenye 

Pia aliialika Zimbabwe kujiunga na mpango uliopendekezwa na rais wa Iran katika Kikao cha 78 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka jana, ambacho alisema kinalenga kulinda familia.

Kadhalika katika mazungumzo yao, viongozi hao wawili waligusia hali ya wanawake wa Kipalestina huko Gaza, na kutaka kukomeshwa jinai za utawala ghasibu wa Israel dhidi ya watu wa eneo hilo linalozingirwa.

Wakati huo huo Datka Ensiyeh Khazali ametoa wito wa kuundwa muungano wa kimataifa ili kukomesha mauaji ya kimbari ya utawala wa Israel dhidi ya watu wa Palestina huko Gaza.

Ametoa maoni hayo wakati wa mkutano na Waziri wa Masuala ya Wanawake wa Nigeria Uju Kennedy Ohanenye, ambao ulifanyika pia pembizoni mwa kikao hicho  cha 68 cha mwaka cha Tume ya Hali ya Wanawake ya Umoja wa Mataifa.

Viongozi hao wawili pia wamebadilishana mawazo kuhusu kuwawezesha wanawake katika hali ya kiuchumi na kijamii, pamoja na njia za kulinda familia katika kukabiliana na vitisho vinavyoweza kutokea.

 

 

Tags