Apr 16, 2024 10:47 UTC
  • Rais wa Afrika Kusini aanza ziara ya kikazi nchini Uganda kujadili suala la DRC

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ambaye aliwasili nchini Uganda jana Jumatatu kwa ziara ya kikazi ya siku mbili, ameendelea na ziara yake hiyo leo Jumanne. Ramaphosa ameelekea nchini Uganda kwa mwaliko rasmi wa Rais Yoweri Museveni.

Madhumuni ya ziara ya Ramaphosa ni kuimarisha uhusiano bora uliopo kati ya nchi zao mbili na kujadiliana usalama na utulivu wa kikanda, ikiwa ni pamoja na hali ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Afrika Kusini ni moja ya vyanzo vinavyokua kwa kasi vya uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni kwa Uganda na pia ni kivutio cha madaktari wengi waliopata mafunzo nchini Uganda.

Mwezi Februari mwaka jana, Rais Museveni alitembelea Afrika Kusini katika safari ambayo ilijikita zaidi kwenye masuala ya uwekezaji na utulivu nchini DRC.

Katika ziara yake hiyo, Museveni alisema kuwa, watashirikiana na Afrika Kusini kutatua tatizo la usalama mashariki mwa DRC linalohusisha waasi wa M23 na wale wa Uganda Allied Democratic Forces au ADF.

Rais Museveni pia alisema kuwa, Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hapaswi kufanya kazi na madola ajinabi akikusudia nchi za Magharibi na wafuasi wao, ambao aliwaita ni wasaliti. Museveni pia amekuwa akipinga kupelekwa askari wa Umoja wa Mataifa huko mashariki mwa DRC.

Mwaka jana, Ujumbe wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (SAMIDRC), ambapo DRC ni mwanachama, uliidhinisha kupelekwa askari wa SADC nchini Congo ili kuisaidia Kinshasa kuleta utulivu na kukabiliana na genge la waasi la M23.