Jun 05, 2024 13:03 UTC
  • Viongozi wa Kiislamu Tanzania walaani vitendo vya ushoga

Viongozi wa dini ya Kiislamu nchini Tanzania wameendelea kukemea vitendo vya ushoga vinavyooenekana kushamiri katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Sheikh Alhad Mussa ambaye ni Mwenyekiti wa Maridhiano na Amani Tanzania, ameitaka serikali kuchunguza sakata la ushoga linalodaiwa kufanyika katika Hoteli ya Ramada jijini Dar es Salaam.

Alhad ametoa mwito huo katika mkutano wa Semina ya Viongozi wa Jumuiya uliofanyika katika ukumbi wa JNICC Posta jijini Dar es Salaam, ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda.

Alhad ambaye amewahi kuwa Sheikh Mkuu wa Dar es Salaam amesisitiza kuwa: "Tutaendelea kupinga machafu yote yanayoendelea katika Nchi yetu, hasa  jambo la Ushoga. Jambo ambalo halikubali na Watanzania, hata serikali yetu imesimama imara."

Huko nyuma pia, Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Zuberi, alisema ushoga haukubaliki nchini Tanzania na unatakiwa kupingwa kwa nguvu zote. “Jambo la ushoga halikubaliki, haiwezekani nchi tukufu kama Tanzania kuwa na vitendo hivi. Masheikh lisemeni jambo hili ili tunusuru umma na taifa kwa ujumla.” Alisema Mufti wa Tanzania. 

Wakati huo huo, Hoteli ya Ramada Resort ya Dar es Salaam imetoa tamko dhidi ya 'uvumi' ulionea kuhusu kujihusisha na mtandao wa LGBTQ (Pan Africa ILGA).

Uvumi huo ulioenea kupitia mtandao wa X ulikuwa kwenye barua iliyokuwa ikiashiria kumshukuru na kumpongeza mmoja wa viongozi wa Ramada Resort kwa kuwalinda wanajamii wa LGBTQ.

Hata hivyo kupitia mtandao wa X, Pan Africa ILGA imekanusha kwamba barua hiyo haijatoka kwao na ni uvumi uliotengenezwa na watu wenye nia mbaya.

Tags