UNICEF yatoa mwito wa uwekezaji wa elimu kwa watoto Afrika
Siku ya Mtoto wa Afrika inaadhimishwa kesho Jumapili. Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limesema kuwa, uwekezaji mkubwa katika elimu ya msingi kwa watoto wa Afrika unahitajika ili kulisaidia bara hilo kutimiza ajenda yake ya muda mrefu ya ustawi na mabadiliko.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa aidha limesema: Ufadhili wa elimu barani Afrika ni mbaya mno kiasi kwamba, kati ya kila nchi tano, ni wastani wa chini ya nchi moja iliyojitolea kuwekeza kwa asilimia 20 ya bajeti yake katika kuimarisha ujuzi wa msingi kwa watoto wao.
Kaulimbiu ya Siku ya Mtoto wa Afrika ya mwaka huu wa 2024, ambayo huadhimishwa Juni 16 kila mwaka, itakuwa "Elimu kwa watoto wote barani Afrika: wakati ni sasa."
UNICEF imesema kuwa, licha ya jukumu lake la kujenga mtaji wa watu ili kukuza ustawi barani Afrika, ufadhili wa elimu katika bara hilo umedorora, na hivyo kuwazuia mamilioni ya watoto kupata elimu ya msingi na ujuzi ambao wanahitaji kuweza kustawi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, juhudi kubwa za serikali za Afrika katika muongo mmoja uliopita ni kuongeza uandikishaji wa wanafunzi wa skuli za msingi na sekondari, lakini skuli zinaendelea kukosa huduma za kimsingi, zina msongamano mkubwa wa wanafunzi, na hazina walimu wa kutosha.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limebainisha kuwa wanne kati ya kila watoto watano wa Afrika wenye umri wa miaka 10 hawawezi kusoma na kuelewa maandishi mepesi tu, na hayo ni matokeo ya uduni wa elimu barani humo.