UNHCR: Kenya hivi sasa ina wakimbizi 775,000 kutoka zaidi ya nchi 20 tofauti
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa limesema kuwa, Kenya ina wastani wa wakimbizi 775,000 na wanaotafuta hifadhi kutoka zaidi ya nchi 20 tofauti duniani.
Hayo yamesemwa na Nanduri Sateesh, mkuu wa Ofisi Ndogo ya Kambi ya Wakimbizi ya Kakma ya shirika hilo la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) na kuongeza kuwa, kwa hivi sasa wakimbizi 100,000 wanaishi katika maeneo ya mijini.
Akiwa katika kambi hiyo ya wakimbizi, Sateesh amesema: "Takriban asilimia 90 ya wakimbizi katika kambi hii wanatokea Somalia, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Ethiopia na Burundi."
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, kambi za wakimbizi za Dadaab ya kaskazini mashariki mwa Kenya ina wakimbizi 375,000, wakati kambi ya wakimbizi ya Kakma ina takriban wakimbizi 288,000.
Ameongeza kuwa, takriban miaka mitano iliyopita, idadi ya wakimbizi ilikuwa 500,000, lakini idadi hiyo imekuwa ikiongezeka kutokana na kukosekana utulivu katika eneo la mashariki mwa Afrika.
Afisa huyo wa UNHCR amesisitiza pia kuwa, wakimbizi wamekuwa wakimiminika nchini Kenya kutokana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa kama vile ukame katika nchi zao.