Iran yakataa takwa la EU la kujadili kusitisha mpango wake wa nyuklia
(last modified Thu, 03 Jul 2025 04:39:42 GMT )
Jul 03, 2025 04:39 UTC
  • Iran yakataa takwa la EU la kujadili kusitisha mpango wake wa nyuklia

Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amepinga msimamo wa Umoja wa Ulaya (EU) wa hivi karibuni unaotaka kuanzishwa mazungumzo mapya yenye lengo la kusitisha mpango wa nyuklia wa Iran.

Taarifa hiyo ilitolewa Jumatano, kufuatia kauli ya Mkuu wa Sera za Kigeni wa EU, Kaja Kallas, aliyetoa wito Jumanne kwa Iran kushiriki mara moja katika mazungumzo ya kuzuia shughuli zake za nyuklia.

Kupitia chapisho kwenye mtandao wa X, Araghchi alieleza kuwa Kallas amepuuza misingi ya Mkataba wa Kuzuia Ueneaji wa Silaha za Nyuklia (NPT), unaotambua haki ya kila nchi mwanachama, ikiwa ni pamoja na Iran, kuendeleza, kufanya utafiti na kutumia teknolojia ya nyuklia kwa madhumuni ya amani.

Amesema kuwa wito wa EU ni ukiukwaji wa haki ya Iran ya kujitawala chini ya sheria za kimataifa, na hauzingatii ugumu wa makubaliano ya awali ya nyuklia.

Araghchi amekosoa msimamo wa EU kwa kurejelea Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa namba 2231, ambalo liliridhia Mkataba wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) wa mwaka 2015, unaojulikana  kama makubaliano ya nyuklia ya Iran.

Araghchi amekataa ushiriki wowote wa Umoja wa Ulaya na Uingereza katika mazungumzo yoyote yajayo, akisema kuwa mchango wao sasa hauna maana wala mashiko, hasa kutokana na uhalisia wa kisiasa ulivyo.

Tangu Marekani ijiondoe kwenye mapatano ya JCPOA  mwaka 2018 na kuiwekea Iran vikwazo vikali vipya, Jamhuri ya Kiislamu imeongeza juhudi za kutetea haki yake ya kutumia teknolojia ya nyuklia, kwa kusisitiza kuwa mpango wake unalenga matumizi ya amani kama vile uzalishaji wa nishati na utafiti wa kimatibabu.

EU, pamoja na Ufaransa, Ujerumani na Uingereza (wanaofahamika kwa pamoja kama E3), zimekuwa zikijitahidi kuhuisha JCPOA kwa njia za kidiplomasia. Hata hivyo, Tehran imekuwa ikilalamikia kwa muda mrefu kile inachokiita “kutokuwepo kwa hatua halisi na pia undumakuwili” wa nchi za Ulaya tangu Marekani ijiondoe kwenye mkataba huo.

Araghchi  alionya Jumanne kuwa hatua za EU za kuishinikiza Iran pamoja na kuunga mkono sera za uchokozi za Israel, ambazo zinaungwa mkono na baadhi ya nchi za Ulaya , zinaweza kuharibu zaidi hali na kuzuia juhudi zozote za kidiplomasia.

Amesema kuwa mienendo kama hiyo ni hatari, na inakwamisha mazingira ya mazungumzo ya haki na yenye kuheshimu usawa wa kimataifa.