Sudan: Hatujawahi kuuomba msamaha Muungano wa Falme za Kiarabu (Imarati)
Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imekanusha habari zinazodai kuwa Khartoum imeuomba radhi Muungano wa Falme za Kiarabu (Imarati) baada ya mwakilishi wa kudumu wa Sudan katika Umoja wa Mataifa kuishutumu Imarati kwa kuvisaidia vikosi vya RSF.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imesema katika taarifa yake kwamba, kuna baadhi ya vyombo vya habari vinaeneza uvumi na taarifa za uwongo vikijifanya kunukuu duru isiyojulikana ikidai kwamba balozi wa Sudan huko Abu Dhabi ameiomba radhi mamlaka ya Imarati lakini uvumi huo hauna mashiko wala ukweli wowote.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imesisitiza kuwa, madai hayo yako mbali kabisa na ukweli hasa kwa kuzingatia kuwa, matamshi yaliyotolewa na Balozi Harith Idris katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni msimamo rasmi wa Sudan kuhusu suala lililokuwa linajadiliwa katika kikao hicho cha Baraza la Usalama.
Jumanne iliyopita, mwakilishi wa Sudan katika Umoja wa Mataifa na wakati mkutano wa wazi Baraza la Usalama ulipokuwa unaendelea kwa ajili ya kusikiliza ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Sudan, aliishutumu Imarati na vikosi vya Libya vyenye mfungamano na Jenerali mstaafu Khalifa Haftar kwa kufanya magendo ya silaha na watu ndani ya Sudan kwa ajili ya kuwasaidia wanamgambo wa RSF.
Balozi Idris alisema: Mashambulizi ya RSF yanafanywa kwa msaada wa silaha wa Imarati. Mashambulizi hayo yanalenga kwa makusudi vijiji na miji na kutumia vibaya udhaifu wa ya Baraza la Usalama ambalo limeshindwa kuchukua msimamo thabiti dhidi yao.
Aliongeza kuwa, Muungano wa Falme za Kiarabu unawasaidia wanamgambo wa RSF kupitia mipaka ya Chad, kusini mwa Libya na Jamhuri ya Afrika ya Kati.