Libya yaitisha kongamano la Nchi zinazopakana na Bahari ya Medeterania kuhusu suala la uhamiaji
Viongozi wa Ulaya na Afrika walikutana nchini Libya jana Jumatano katika Kongamano la Wahamiaji Wanaovuka Bahari ya Mediterania ikiwa ni katika juhudi za kutafuta suluhisho la mgogoro wa wimbi kubwa la wahamiaji haramu wanaotumia bahari hiyo.
Kongamano hilo limeitishwa ili kukusanya pamoja naoni na mitazamo ambayo itaongeza ushirikiano na uratibu kati ya nchi husika kwa ajili ya kuwa na misingi ya uchumi endelevu na uhusiano wa kibiashara baina ya Ulaya na Afrika.
Akizungumza kwenye kongamano hilo, Waziri Mkuu wa Libya Abdul-Hamed Dbeibah ametoa mwito wa kuhamasishwa upya wafadhali ili watoe fedha za kusimamia na kudhibiti wimbi lisilo la kawaida wa uhamiaji haramu kupitia njia mbalimbali zikiwemo za kufadhili miradi ya maendeleo katika nchi za Afrika wanakotokea wahamiaji hao ili kupunguza vishawishi vya kukimbia nchi zao.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Libya LANA, Dbeibah ametoa mwito huo akisema: “Tutekeleze miradi ya kweli yenye kuleta utulivu kwa wananchi wa nchi hizi na kuwafanya wabakie katika maeneo yao.”
Kwa upande wake, Rais Mahamat Idriss Deby Itno wa Chad ametoa mwito wa kuongezwa juhudi za kutafutia ufumbuzi uhamiaji usio wa kawaida, kutambua sababu zake na kushughulikia suala hilo kwa kuzingatia haki za binadamu.
Naye Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni amesema kuwa, nchi yake inalipa kipaumbele kikubwa suala la kukabiliana na wimbi kubwa la wahamiaji wasio wa kawaida na inatilia mkazo wajibu wa kuimarishwa juhudi na nchi za eneo hilo katika vita vya kupambana na wimbi hilo.