Mapigano yaendelea katikati ya mji wa Sirte, Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i11431-mapigano_yaendelea_katikati_ya_mji_wa_sirte_libya
Mapigano baina ya serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya na genge la kigaidi la Daesh yangali yanaendelea katikati ya mji wa Sirte, kaskazini mwa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 17, 2016 11:23 UTC
  • Mapigano yaendelea katikati ya mji wa Sirte, Libya

Mapigano baina ya serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya na genge la kigaidi la Daesh yangali yanaendelea katikati ya mji wa Sirte, kaskazini mwa nchi hiyo.

Mashirika ya habari yamemnukuuu Ridha Isa, msemaji wa askari wa Misrata katika mji wa Sirte akisema leo Jumapili kuwa, vikosi vya serikali vinasonga mbele kwa mwendo wa kinyonga kutokana na kujaa mabomu ya kutegwa ardhini vile vile kuweko magaidi wanaotungua watu kwa risasi kutokea mbali.

Ameongeza kuwa askari wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya wanaendelea kushambulia kwa mizinga na kwa mashambulizi ya anga; maeneo ya magaidi wa Daesh pembeni mwa jengo la Ouagadougou katika eneo la Giza al Askariya katikati ya mji wa Sirte.

Habari zinasema kuwa, mapigano yanayoendelea katikati ya mji wa Sirte yamepelekea wanajeshi saba wa serikali kuuawa na 49 wengine kujeruhiwa.

Hata hivyo magaidi wa Daesh wamezingirwa katikati ya mji wa Sirte baada ya serikali ya umoja wa kitaifa kuanzisha opereseheni ya kuuokomboa mji huo muhimu ambao Daesh imeufanya kuwa ngome yake kuu.

Iwapo mji wa Sirte utakombolewa kikamilifu, litakuwa ni pigo kubwa kwa magaidi wa Daesh na ndio maana wanatumia nguvu zao zote kuzorotesha ukombozi wa mji huo.

Mwaka mmoja nyuma, kundi la Daesh lilijipenyeza ndani ya Libya kutokana na kutokuweko serikali moja yenye nguvu nchini humo, na kuteka baadhi ya maeneo ukiwemo mji wa bandari wa Sirte.