Afrika Kusini yailaani Israel kwa kumuua kigaidi Ismail Haniyah
Serikali ya Afrika Kusini imelaani vikali mauaji ya kigaidi ya Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS, Ismail Haniyah.
Wizara ya Uhusiano na Ushirikiano wa Kimataifa ya Afrika Kusini jana Alkhamisi ilitoa taarifa rasmi na kulaani vikali mauaji hayo ya kigaidi dhidi ya Haniyah aliyekuwa ziarani hapa Tehran, yaliyofanywa na Israel Jumatano asubuhi (Julai 31).
Taarifa ya Wizara hiyo ya mambo ya nje ya Afrika Kusini imesema: Serikali (ya Pretoria) inatoa rambirambi zake za dhati kwa familia ya Haniyah, uongozi (wa HAMAS) na watu wa Palestina.
"Afrika Kusini ina wasiwasi kwamba mauaji ya Dakta Haniyah na kuendelea kuwalenga raia huko Gaza kutashadidisha zaidi hali ya wasiwasi katika eneo zima," imeeleza taarifa hiyo.
Imeongeza kuwa, "Afrika Kusini inataka uchunguzi wa kina ufanywe na kutoa wito kwa pande zote kujizuia kwa hali ya juu ili kuepuka vitendo vyovyote vinavyoweza kuzidisha hali ya wasiwasi katika eneo hilo tete."
Taarifa hiyo iliyotiwa saini na Waziri wa Uhusiano na Ushirikiano wa Kimataifa wa Afrika Kusini, Ronald Lamola imebainisha kuwa, "Vitendo kama hivyo vya mauaji ya kiholela vinakiuka sheria za kimataifa na kanuni za haki za binadamu, na kudhoofisha juhudi za kimataifa za kuimarisha amani na utulivu katika eneo la Mashariki ya Kati."
Afrika Kusini imeashiria mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na Israel dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza na kusisitiza kuwa, hakuna kitu kinachoweza kuhalalisha mauaji hayo ya kimakusudi ambayo hayajawahi kuhuhudiwa katika historia ya hivi karibuni.