Kituo cha mwisho cha jeshi la Marekani nchini Niger chafungwa
Aug 05, 2024 10:21 UTC
Kambi ya mwisho ya kijeshi ya Marekani nchini Niger imekabidhiwa rasmi leo kwa nchi hiyo ya Afrika.
Kambi ya mwisho ya kijeshi ya Marekani nchini Niger imekabidhiwa leo Jumatatu kwa nchi hiyo ya Kiafrika huku nchi tatu za Niger, Mali na Burkina Faso zikipanga kuunda kikosi cha pamoja cha kuwatimua wanajeshi wa kigeni, wakiwemo wa Marekani.
Kuondolewa wanajeshi wa kigeni ni sehemu ya mpango mkubwa wa kuviondoa vikosi vya majeshi ya nchi za Magharibi katika eneo la Sahel barani Afrika.
Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB, Marekani itakabidhi kambi yake ya kijeshi kwa mamlaka husika ya Niger leo kulingana na makubaliano iliyofikia na mamlaka hiyo.
Kulingana na makubaliano hayo, Septemba 15 iliwekwa kama tarehe ya mwisho ya kuondoka wanajeshi wa Marekani nchini Niger.
Kambi ya 201 ya anga iliyoko katika mji wa Agadez ni moja ya kambi mbili za Marekani ambazo zilianzishwa kwa kile eti kilichoitwa 'operesheni za kupambana na ugaidi nchini Niger'.
Mwezi uliopita, wanajeshi wa Marekani waliondoka kwenye kambi ndogo ya ndege zisizo na rubani ya 101 iliyoko katika mji mkuu wa Niger, Niamey.
Wanajeshi wa Ujerumani pia wamepangiwa kuondoka mwezi huu katika kambi ya kijeshi nchini Niger.
Anneliese Bernard, Mkurugenzi wa Kituo cha Ushauri wa Uthabiti wa Kimkakati kilichoko Washington, ambacho kijahusisha na masuala ya maeneo ya Sahel na Pwani za Magharibi mwa Afrika amesema kuhusiana na kuondolewa wanajeshi wa kigeni nchini Niger kwamba, kuondolewa wanajeshi hao kunaweza kusababisha ombwe kubwa la usalama katika nchi hiyo.../