Aug 14, 2024 08:11 UTC
  • Mahakama ya Uganda yamkuta na hatia kiongozi wa waasi wa LRA

Mahakama nchini Uganda jana ilimpata na hatia kamanda wa zamani wa kundi la Waasi wa Kikristo la kaskazini mwa Uganda (LRA). Thomas Kwoyelo amepatikana na hatia kwa kuhusika katika makosa kadhaa ya jinai dhidi ya binadamu katika kesi ya kwanza ya jinai za kivita kusikilizwa katika nchi hiyo ya mashariki mwa Afrika.

Thomas Kwoyelo ambaye alishtakiwa kwa uhalifu uliofanywa wakati wa uasi wa umwagaji damu wa miongo miwili wa kundi la LRA kaskazini Uganda, alikuwa akisubiri kwa miaka kadhaa gerezani kuhukumiwa katika kesi hiyo muhimu iliyokuwa ikimkabili.

Jaji Michael Elubu wa kitengo cha Kimataifa cha Uhalifu katika Mahakama Kuu katika mji wa Gulu kaskazini mwa Uganda amesema kuwa kamanda huyo wa zamani wa kundi la LRA amepatikana na hatia ya makosa 44 na kuhukumiwa na kwamba hakukutwa na hatia ya makosa matatu ya mauaji na makosa mengine 31 yaliyokuwa yakimkabili yametupiliwa mbali.  

Thomas Kwoyelo ambaye alitekwanyara na kundi la waasi wa Kikristo la LRA akiwa na umri wa miaka 12 amekanusha tuhuma zote dhidi yake. Alikamatwa mwezi Machi mwaka 2009 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakati wa oparesheni ya vikosi vya ulinzi vya eneo dhidi ya waasi wa LRA ambao walikimbilai huko wakitokea Uganda miaka miwili nyuma. 

 

Tags