Wanaharakati waitaka Afrika Kusini iiwekee Israel vikwazo vya biashara
Wanaharakati wameitaka Afrika Kusini iuwekee utawala wa Kizayuni wa Israel vikwazo vya kibiashara na kusimamisha mara moja mauzo ya nje ya bidhaa zake kwa utawala huo pandikizi.
Wanaharakati hao wamesema juhudi za Afrika Kusini za kutaka Israel iwajibishwe katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki hazitoshi, na wameitaka serikali yao kukata uhusiano wote wa kibiashara na Tel Aviv.
Abeeda Adams, mwanachama wa 'Kampeni ya Mshikamano na Palestina' amesema, kwa kuiuzia Israel makaa ya mawe, Afrika Kusini inasaidia na kuunga mkono mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza.
Amesema: Tunaamini kwamba, uhusiano wowote wa kiuchumi au mwingine wowote ulio nao na dola la Israeli unachangia mauaji ya kimbari yanayofanywa na serikali ya kibaguzi ya Israel.
Afrika Kusini ndiyo mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara na Israel barani Afrika, na katika kipindi cha miezi minane iliyopita, imesafirisha zaidi ya tani 500,000 za makaa ya mawe kwa utawala huo katili. Wanaharakati hao wamesema makaa ya mawe ya Afrika Kusini yanachangia 15% ya gridi ya umeme ya Israeli, na kwamba Pretoria inapasa kukomesha mara moja upelekaji wa bidhaa hiyo kwa Israel.
Ikumbukwe kuwa, Novemba mwaka jana, Afrika Kusini ilitangaza kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na utawala wa Kizayuni wa Israel, kufuatia kuendelea jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya taifa la Palestina.
Tangu kuanza vita vya Gaza Oktoba mwaka jana na kushadidi mauaji ya Wapalestina yanayofanywa na Israel, Afrika Kusini imekuwa ikitoa kauli za kulaani jinai za Israel na kutoa wito wa kukomeshwa mara moja vita huko Gaza.