Israel: Hatusitishi mashambulizi mpaka Wapalestina wafukuzwe Gaza; Syria igawanyishwe
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i125818-israel_hatusitishi_mashambulizi_mpaka_wapalestina_wafukuzwe_gaza_syria_igawanyishwe
Waziri wa fedha mwenye misimamo ya kuchupa mipaka wa Israel, Bezalel Smotrich anasema utawala huo wa Kizayuni utasitisha tu uvamizi wake Gaza wakati "mamia ya maelfu" ya Wapalestina watalazimishwa kuyahama makazi yao; na Syria igawanyishwe vipande vipande.
(last modified 2025-04-30T10:19:51+00:00 )
Apr 30, 2025 10:19 UTC
  • Israel: Hatusitishi mashambulizi mpaka Wapalestina wafukuzwe Gaza; Syria igawanyishwe

Waziri wa fedha mwenye misimamo ya kuchupa mipaka wa Israel, Bezalel Smotrich anasema utawala huo wa Kizayuni utasitisha tu uvamizi wake Gaza wakati "mamia ya maelfu" ya Wapalestina watalazimishwa kuyahama makazi yao; na Syria igawanyishwe vipande vipande.

"Tutahitimisha kampeni hii ... wakati Gaza itakaposafishwa na kuondokana na Hamas na mamia ya maelfu ya watu wa Gaza watakapokuwa njiani kutoka humo kuelekea nchi nyingine," Smotrich amesema hayo katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.

Press TV imeandika habari hiyo na kueleza kuwa, matamshi ya mwanasiasa huyo mwenye misimami mikali wa Israel yanadhihirisha ukaidi wa utawala huo ghasibu wa wa kutekeleza kivitendo mpango wake wa kuwahamisha Wapalestina kwa lazima kutoka Ukanda wa Gaza, jambo lililopendekezwa kwa mara ya kwanza na Rais Donald Trump wa Marekani.

Ikishajiishwa na tangazo hilo la Trump, Israel ilianzisha tena vita vyake vya umwagaji damu dhidi ya Wapalestina wa Gaza mwezi Machi, na kukiuka makubaliano ya usitishaji vita yaliyosimamiwa na Marekani. Tangu wakati huo, imekuwa ikiishambulia Gaza kwa mabomu, na kulifanya eneo hilo kutoweza kukalika, ikiwa ni katika jitihada za kuwalazimisha Wapalestina kuondoka humo.

Kadhalika, kwa muda wa siku 50 zilizopita, utawala haramu wa Israel umezuia misaada ya kibinadamu kuingia Gaza, ambako mamia ya raia wameuawa katika mashambulizi makali. Utawala huo pandikizi pia umezishawishi baadhi ya nchi kuwakubali Wapalestina waliofurushwa kwa nguvu Gaza.

Jinai za Israel Ukanda wa Gaza

Katika matamshi yake, Smotrich ametoa wito kwa Harakati ya Muqawama ya Lebanon Hizbullah "kushambuliwa vikali," kuashiria kuwa Israel ina azma ya kuyabakisha majeshi yake kusini mwa Lebanon.

Aidha ametoa wito kwa Syria kugawanywa vipande vipande kama taifa, katika hali ambayo kiongozi wa kundi la wanamgambo la Hay-at Tahrir al-Sham, Abu Mohammed al-Jolani amedokeza kwamba Syria "itaanzisha uhusiano rasmi wa kidiplomasia" na utawala wa Kizayuni wa Israel, itautambua utawala huo, na kubadilishana nao mabalozi ifikapo mwisho wa mwaka ujao wa 2026, eti kwa masharti maalum.