Umoja wa Mataifa walalamikia maamuzi ya upande mmoja yanayohatarisha amani nchini Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i115712-umoja_wa_mataifa_walalamikia_maamuzi_ya_upande_mmoja_yanayohatarisha_amani_nchini_libya
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya (UNSMIL) umelalamikia uamuzi wa upande mmoja wa Benki Kuu ya Libya hasa wakati huu ambapo hali inazidi kuwa mbaya nchini humo kutokana na maamuzi ya upande mmoja ya mirengo kisiasa.
(last modified 2024-08-28T00:49:41+00:00 )
Aug 28, 2024 00:49 UTC
  • Umoja wa Mataifa walalamikia maamuzi ya upande mmoja yanayohatarisha amani nchini Libya

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya (UNSMIL) umelalamikia uamuzi wa upande mmoja wa Benki Kuu ya Libya hasa wakati huu ambapo hali inazidi kuwa mbaya nchini humo kutokana na maamuzi ya upande mmoja ya mirengo kisiasa.

Kauli hiyo ya Umoja wa Mataifa imekuja kufuatia serikali yenye makao yake mashariki mwa nchi kufunga maeneo ya mafuta na bandari ili kulipiza kisasi jaribio la serikali ya magharibi mwa nchi hiyo la kuidhibiti Benki Kuu bila ya kushirikisha upande wa pili. 

Katika taarifa yake, UNSMIL imeonya kwamba kusuluhisha mgogoro huu kutakuwa na gharama kubwa kwa Walibya na kunaweza kuporomosha uchumi wa nchi hiyo.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, UNSMIL inaitisha mkutano wa dharura kwa pande zote zinazohusika katika mzozo huo ili kujaribu kufikia muafaka na inatoa mwito wa kusimamishwa maamuzi yote ya upande mmoja kuhusiana na Benki Kuu na kufungwa visima vya mafuta. 

Baraza la Uongozi lenye makao yake magharibi mwa Libya hivi karibu liliteua gavana mpya wa Benki Kuu, lakini Baraza la Wawakilishi lenye makao yake makuu mashariki mwa Libya lilikataa uamuzi huo likisema kwamba uko nje ya mamlaka ya baraza hilo la magharibi mwa nchi.

Siku ya Jumapili, vyombo vya habari vya ndani ya Libya viliripoti kwamba kamati kutoka Baraza la Uongozi ilijaribu kuingia katika makao makuu ya Benki Kuu mjini Tripoli kutekeleza uamuzi wake huo wa kuteua Gavana wa benki hiyo bila ya ridhaa ya serikali ya upande wa mashariki.

Tangu alipopinduliwa Muammar Gaddafi mwaka 2011, Libya imekumbwa na mgawanyiko huku kukiwa na serikali mbili, moja iko upande wa mashariki na nyingine upande wa magharibi mwa nchi hiyo.