China yaionya Marekani kuhusu mauzo ya silaha kwa Taiwan
-
Xi Jinping
China kwa mara nyingine tena imepinga vikali hatua ya Marekani kuzidisha himaya na uungaji mkono wake wa kijeshi kwa Taiwan sambamba na ziara ya Rais Trump mjini Beijing.
China imeitaka Washington iheshimu ahadi zake za muda mrefu kwa mujibu wa sera ya "China Moja".
Trump yuko ziarani huko Beijing iliyoanza Mei 13 na itakayoendelea hadi Ijumaa Mei 15. Hii ni ziara ya kwanza kufanywa na Rais wa Marekani nchini China tangu mwaka 2017 wakati Trump alipokutana na Rais Xi Jinping katika muhula wake wa kwanza wa urais.
China ina mamlaka ya utawala kwa Taiwan, na kwa mujibu wa Sera ya " China Moja", karibu nchi zote, ikiwemo Marekani, zinatambua mamlaka hiyo.
Ajenda kuu ya mazungumzo ya Marais wa China na Marekani ni kuhusu mvutano juu ya Taiwan baada ya serikali ya Trump kuidhinisha kifurushi za mauzo ya silaha ya dola bilioni 11 kwa Taiwan; kiwango ambacho kimetajwa kuwa kikubwa.
Maafisa wa China wameendelea kusisitiza kuwa Taiwan inasalia kuwa suala la ndani na wamelaani ushirikiano wote wa kijeshi kati ya kisiwa hicho na Washington, ambayo haina uhusiano rasmi wa kidiplomasia na kisiwa hicho.
"Tunapinga vikali Marekani kujihusisha na aina yoyote ya uhusiano wa kijeshi na eneo la China la Taiwan, na tunapinga hatua ya Marekani kuiuzia silaha Taiwan ambayo iko chini ya mamlaka ya China. Msimamo huu ni thabiti na hauna shaka," amesema Zhang Han, Msemaji wa Baraza la Serikali la Ofisi ya Masuala ya Taiwan wakati wa mkutano wa kawaida wa wanahabari mjini Beijing.