Raila atangaza rasmi kuwania uenyekiti wa Umoja wa Afrika
-
Raila Odinga
Raila Odinga, Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya na kiongozi wa upinzani jana Jumanne alitangaza rasmi kugombea uenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU).
Raila ametangaza hayo wakati wa uzinduzi rasmi wa kampeni yake mjini Nairobi ambao umehudhuriwa na viongozi wa kikanda kutoka sehemu mbalimbali za bara la Afrika na kuelezea mtazamo wake kuhusu namna ya kuifanya AU kuwa amilifu zaidi.
Uchaguzi wa mwenyekiti na nyadhifa nyingine saba za AU utafanyika wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Umoja wa Afrika mwezi Februari 2025. Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika anahudumu kwa muda wa miaka minne ambao unaweza kuongezewa muda mara moja.
Katika sehemu moja Raila Odinga amesema: "Nina ndoto ya Afrika ambayo mipaka na lugha za kikoloni hazitotutenganisha tena. Waafrika lazima tuwe na umoja, tuwe watu wenye ujasiri na matumaini ya mustakabali mzuri kupitia kuwatumia vizuri vijana wetu."
Kwa mujibu wa shirika la habari la Anadolu, wachambuzi wa kisiasa wanaona kuwa, hatua hiyo ya Odinga ni aina fulani ya kichocheo cha mabadiliko ndani ya Umoja wa Afrika kutokana na harakati zake za muda mrefu za kupigania utawala wa kidemokrasia na uadilifu katika jamii.
Shirika hilo la habari limemnukuu Simon Mukhwana, mchambuzi wa masuala ya kisiasa akisema jijini Nairobi kwamba: "Ahadi ya Odinga ya kuifanya AU ijikite zaidi kwa watu ni ahadi kabambe na ina uwezo wa kuongeza kwa kiasi kikubwa itibari ya umoja huo. Changamoto itakuwa ni kutafsiri kivitendo ahadi hizi na kuwa na athari chanya katika maisha ya kila siku ya Waafrika."