Wiki za mafuriko nchini Nigeria, kwa uchache watu 170 wamethibitishwa kupoteza maisha
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i115726-wiki_za_mafuriko_nchini_nigeria_kwa_uchache_watu_170_wamethibitishwa_kupoteza_maisha
Takriban watu 170 wamethibitishwa kupoteza maisha na karibu 2,000 wamejeruhiwa katika matukio yanayohusiana na mvua na mafuriko kwenye kona zote za Nigeria katika kipindi cha wiki mbili za mafuriko. Zaidi ya watu 205,300 wamelazimika kuhama makazi yao.
(last modified 2024-08-28T02:54:44+00:00 )
Aug 28, 2024 02:54 UTC
  • Wiki za mafuriko nchini Nigeria, kwa uchache watu 170 wamethibitishwa kupoteza maisha

Takriban watu 170 wamethibitishwa kupoteza maisha na karibu 2,000 wamejeruhiwa katika matukio yanayohusiana na mvua na mafuriko kwenye kona zote za Nigeria katika kipindi cha wiki mbili za mafuriko. Zaidi ya watu 205,300 wamelazimika kuhama makazi yao.

Kwa mujibu wa takwimu za karibuni kabisa zilizotolewa jana Jumanne na Wakala wa Kitaifa wa Kusimamia Matukio ya Dharura Nigeria (NEMA), hadi wakati wa kutolewa taarifa hii, watu 170 walikuwa wameshapoteza maisha, 1,941 wamejeruhiwa, na 205,338 wamekimbia makazi yao katika karibu majimbo yote ya nchi hiyo.

Majimbo manane katika eneo la kaskazini mwa Nigeria ndiyo yaliyoathiriwa zaidi, huku mvua ikiendelea kunyesha katika mikoa kadhaa. Mamlaka ya hali ya hewa ya nchi hiyo imetabiri kuwa mvua itaendelea kunyesha pia mwezi ujao.

Mafuriko pia yamesomba mimea kwenye makumi ya maelfu ya hekta za ardhi, na kuzua wasiwasi wa janga la njaa na ukosefu wa chakula katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Ahmad Saleh, mkulima wa nafaka wa Jimbo la Yobe la kaskazini mashariki mwa Nigeria amesema kuwa, wakulima wengi wana wasiwasi kwamba athari za mafuriko kwenye mashamba yao zitazidisha mgogoro wa chakula nchini humo.

Mafuriko yamesababisha madhara makubwa katika nchi za Afrika Magharibi kama vile Nigeria, Niger, Chad na Burkina Faso, ambazo hata kabla ya mafuriko hayo zilikuwa tayari zina uhaba wa chakula na matatizo ya kiuchumi. 

Kwa mujibu wa Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu (OCHA) nchi za Niger na Chad kama Nigeria, zina matatizo mengi ya kiuchumi na ya wakimbizi kutokana na mafuriko.