Baraza la Usalama kutangaza vikwazo dhidi ya majenerali wa wapiganaji wa RSF
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i115752-baraza_la_usalama_kutangaza_vikwazo_dhidi_ya_majenerali_wa_wapiganaji_wa_rsf
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, linafikiria kutangaza vikwazo dhidi ya majenerali wawili wa kundi la wapiganaji wa RSF nchini Sudan.
(last modified 2024-08-28T23:20:08+00:00 )
Aug 28, 2024 23:20 UTC
  • Baraza la Usalama kutangaza vikwazo dhidi ya majenerali wa wapiganaji wa RSF

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, linafikiria kutangaza vikwazo dhidi ya majenerali wawili wa kundi la wapiganaji wa RSF nchini Sudan.

Kamati ya baraza hilo inasema kuwa, majenerali hao wanatishia ustawi wa amani ya nchi hiyo pamoja na kuhusika na vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu.

Ikiwa vikwazo hivi vitapitishwa, vitakuwa ni vya kwanza katika vita inayoendelea kati ya jeshi la serikali na wapiganaji wa RSF.

Tayari Marekani imependekeza vikwazo vya kusafiri na kuzuiwa kwa mali za mkuu wa operesheni za kijeshi wa kundi hilo, Osman Mohamed na kamanda Wake kwenye eneo la Darfur, Abdel Rahman Juma Barkalla.

Ikiwa mpaka ijumaa ya wiki huu, kutakuwa hakuna nchi wanachama itakayojitokeza kuweka pingamizi dhidi ya mapendekezo haya, basi vikwazo hivi vitaanza kutekelezwa.

 

Sudan imekumbwa na vita kati ya jeshi, linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, ambaye ni mkuu wa Baraza la Mpito la Utawala, na kundi la RSF linaloongozwa na makamu wake wa zamani Mohamed Hamdan Daglo.

Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, takriban watu 12,260 wameuawa na zaidi ya 33,000 kujeruhiwa katika vita vilivyoanza Aprili 2023,

Mgogoro wa kibinadamu unaendelea kuwa mbaya zaidi kwani karibu watu milioni 6.8 wamekimbia makazi yao kutafuta usalama nchini Sudan au nchi jirani. Jitihada za kieneo na kimataifa hadi sasa ziimeshindwa kukomesha mapigano hayo.