Ethiopia yaingiwa na kiwewe baada ya jeshi la Misri kuingia Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i115784-ethiopia_yaingiwa_na_kiwewe_baada_ya_jeshi_la_misri_kuingia_somalia
Ethiopia siku ya Jumatano ilijibu kwa hasira taarifa za kuingia jeshi la Misri nchini Somalia, hatua ambayo inaashiria kuenea mvutano baina ya nchi hizo mbili jirani katika Pembe ya Afrika.
(last modified 2024-08-29T08:25:27+00:00 )
Aug 29, 2024 08:25 UTC
  • Ethiopia yaingiwa na kiwewe baada ya jeshi la Misri kuingia Somalia

Ethiopia siku ya Jumatano ilijibu kwa hasira taarifa za kuingia jeshi la Misri nchini Somalia, hatua ambayo inaashiria kuenea mvutano baina ya nchi hizo mbili jirani katika Pembe ya Afrika.

Katika taarifa, serikali ya Ethiopia imeonya kwamba ushirikiano wa Somalia na 'majeshi ya nje' huenda ukavuruga eneo hilo.

Taarifa hiyo kutoka Addis Ababa haikuitaja Misri moja kwa moja, lakini ilisema kipindi cha mpito nchini Somalia kutoka Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (Atmis) hadi Kikosi cha Kusaidia na Kuleta Utulivu cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (Aussom) kinafanyika bila kuzingatia maslahi ya kiusalama katika eneo.

Ethiopia imekuwa mchangiaji wa wanajeshi katika Atmis lakini Somalia imeweka wazi kuwa haitaki nchi hiyo ichangie tena askari katika kikosi cha  Aussom baada ya nchi hizo mbili kutofautiana kuhusu Mkataba wa Makubaliano (MoU) kati ya Ethiopia na  eneo lililojitangazia uhuru na kujitenga la Somalia la Somaliland.

Misri, ambayo tayari ina mzozo na Ethiopia kuhusu bwawa la Mto Nile na Ethiopia, tayari imekubali kupeleka wanajeshi 10,000 nchini Somalia ambapo 5,000 watahudumu katika kikosi cha Umoja wa Afrika na wengine  5,000 watapelekwa katika eneo la Hiiraan linalopakana na Ethiopia. Misri inasema Bwawa la Ethiopia litaathiri vyanzo vyake vya maji. Misri iliwahi kutishia kuwa itadondosha mabomu katika bwawa hilo ambalo inaliona kama tishio kwa usalama wake.

Nao mvutano kati ya Somalia na Ethiopia umekuwa ukiendelea tangu Januari wakati Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed na kiongozi wa Somaliland Muse Bihi Abdi, walipotia saini Mkataba ulioipatia Ethiopia ukodishaji wa miaka 50 kwenye kituo cha jeshi la majini na kufikia bandari ya Berbera ya Somaliland kwa shughuli za kibiashara za baharini. Somalia imepinga mapatano hayo na kusema eneo la Somaliland halina haki ya kutia saini mapatano kama hayo na dola la kigeni.