Sep 04, 2024 02:39 UTC
  • Ufisadi Serikalini unawafanya vijana wengi wa Kiafrika wahajiri na kukimbilia Ughaibuni

Karibu asilimia 60 ya vijana wa Kiafrika wanataka kuzihama nchi zao kwa sababu serikali zao hazishikiki kwa ufisadi. Hayo ni kwa mujibu wa uchunguzi mpya wa maoni uliofanywa kwa vijana katika mataifa 16 ya Afrika.

Matokeo ya uchunguzi huo yaliyotolewa siku ya Jumanne yanaeleza kuwa, vijana katika nchi hizo 16 za Afrika wamesema, ufisadi ni kikwazo kikubwa zaidi cha maendeleo katika nchi zao.

Uchunguzi huo wa maoni ulioendeshwa na Wakfu wa Ichikowitz Family wenye makao yake mjini Johannesburg, Afrika Kusini uliwahoji vijana 5,604 wenye umri wa kati ya miaka 18 na 24 katika nchi za Botswana, Cameroon, Chad, Jamhuri ya Kongo, Ivory Coast, Ethiopia, Gabon, Ghana, Kenya, Malawi, Namibia, Nigeria, Rwanda, Afrika Kusini, Tanzania na Zambia.

Asilimia 83 kati ya vijana hao waliotoa maoni yao walisema wanatiwa wasiwasi na ufisadi uliotawala katika nchi zao, huku asilimia 62 wakisema wanaamini kuwa serikali zao zinashindwa kulishughulikia janga hilo.

Uchunguzi huo wa maoni umeonyesha pia kuwa karibu asilimia 58 ya vijana wanasema "kuna uwezekano mkubwa" au "uwezekano wa kiwango fulani" kwamba watafikiria kuhamia nchi nyingine katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo uliofanywa ana kwa ana na wahusika mnamo Januari na Februari mwaka huu, wasiwasi umeenea kutokana na ufisadi ulioko kwenye nyanja tofauti, ikiwa ni pamoja na serikali kuu, serikali za mitaa, biashara, na vikosi vya polisi.

Wakfu wa Ichikowitz Family umesema, vijana wengi wanataka vikwazo vikali zaidi viwekwe dhidi ya wanasiasa mafisadi, ikiwa ni pamoja na kuwapiga marufuku kugombea nyadhifa za uongozi.

Aidha, 55% ya vijana waliotoa maoni yao wamesema, Afrika inaelekezwa "upande usio sahihi".

Mbali na kulalamikia ufisadi uliotawala katika nchi zao, asilimia 72 ya vijana wa Kiafrika waliohojiwa wameeleza kwamba, wana wasiwasi pia kuhusu athari mbaya ya ushawishi wa kigeni hasa wa kunyonywa na makampuni ya kigeni utajiri wao wa rasilimali za madini kwa kuchimbwa na kusafirishwa nje ya nchi bila ya kuwa na manufaa yoyote kwa wananchi.

Kwa mujibu wa Benki ya Maendeleo Afrika, bara hilo lina idadi ya vijana wapatao milioni 420 wenye umri wa miaka 15 hadi 35, theluthi moja yao wakiwa hawana ajira.

Aidha, ni bara lenye idadi kubwa zaidi ya kizazi cha vijana duniani na inayokua kwa kasi zaidi, huku ikitarajiwa kuongezeka maradufu hadi zaidi ya vijana milioni 830 ifikapo mwaka 2050.../

Tags