Kanusho la Iran kwa madai ya uwongo ya Marekani ya kuhusika katika jaribio la kumuua Trump
(last modified Thu, 18 Jul 2024 10:40:05 GMT )
Jul 18, 2024 10:40 UTC
  • Kanusho la Iran kwa madai ya uwongo ya Marekani ya kuhusika katika jaribio la kumuua Trump

Baada ya tukio la kupigwa risasi Donald Trump, rais wa zamani na mgombea wa chama cha Republican katika uchaguzi wa rais wa Marekani wa 2024, baadhi ya vyombo vya habari vya Marekani kwa mara nyingine vikiendeleza propaganda za chuki dhidi ya Iran (Iranphobia) vilidai kuweko mkono wa Iran katika tukio hilo.

Hatua hiyo imekabiliwa na majibu makali ya Iran. Wakati wa kujiri kampeni za uchaguzi Jumamosi ya tarehe 13 Julai huko Butler, Pennsylvania, kijana mwenye umri wa miaka 20 aliyejulikana kwa jina la Thomas Matthew Crooks alimshambulia Donald kwa risasi kadhaa akiwa umbali wa takribanii makumi ya mita  na risasi moja ikampata sikioni mwanasiasa huyo. Mshambuliaji aliyejaribu kumuua Trump aliuawa papo hapo na polisi wa Marekani katika eneo la tukio, na hivyo kuondoa uwezekano wa kuhojiwa ili kubaini wahusika wa tukio hilo.

Mtandao wa televisheni ya Marekani CNN ulidai siku ya Jumanne kwamba, katika majuma ya hivi karibuni mamlaka za kijasusi za nchi hiyo ziligundua njama inayoweza kufanywa na Iran ya kumuua rais wa zamani wa nchi hiyo, Donald Trump. Hata hivyo, chombo hicho cha habari kilisema kuwa, hakuna uhusiano na mfungamano uliopatikana kati ya suala hili na jaribio la Thomas Matthew Crooks la kumuua Trump wakati wa mkutano wa Pennsylvania.

Akijibu baadhi ya ripoti zisizo na msingi zinazodai kuwa Iran imeshiriki katika jaribio la kumuua Donald Trump, rais wa zamani wa Marekani, mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa tuhuma hizo hazina msingi wowote na kwamba ni za kichochezi.

Trump akitolewa katika eneo la tukio baada ya kupigwa risasi ya sikio

 

Amir Saeid Iravani, mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa mjini New York alisema siku ya Jumanne, akijibu ripoti zinazodai kuwa Iran ilihusika katika jarihio hilo la mauaji, kwamba tukio la kupigwa risasi Trump linaweza kutathminiwa kama ishara nyingine ya kuongezeka kila siku ghasia za kisiasa nchini Marekani katika miaka ya hivi karibuni, hasa baada ya kushambuliwa Bunge la Congress ya Marekani na wafuasi wa Donald Trump Januari tarehe 6, 2021.

Amir Saeid Iravani, amesisitiza kuwa, kwa mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Donald Trump, ni mtendajinai anayepaswa kushtakiwa na kuhukumiwa mahakamani kwa kutoa amri ya kuuawa kigaidi Luteni Jenerali Qassim Soleimani kamanda wa zamani wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (SEPAH), aliyeuawa shahidi Januari 3, 2020. Kuhusiana na suala hilo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imechagua njia ya kisheria ya kumuwajibisha Trump.

Ali Bagheri Kani, Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, siku ya Jumanne, akijibu swali la Fareed Zakaria, mwandishi wa CNN katika mkutano na waandishi wa habari mjini New York, Marekani, kuhusu ufuatiliaji wa mauaji ya Jenerali Qassem Soleimani, ambayo yalifanyika kwa amri ya Rais wa wakati huo wa Marekani, Donald Trump, alisema: "Niliwaambia wazi kwamba, tutafuata taratibu na mifumo ya kisheria na ya kimahakama katika ngazi ya ndani na kimataifa ili kuwakabidhi kwa mikono ya sheria wahusika na washauri wa kijeshi wa mauaji ya Qassim Soleimani. Wakati huo huo, Nasser Kan'ani", msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran, naye alikanusha na kupuuza  ripoti ya moja ya vyombo vya habari vya Marekani inayodai kuhusika Iran katika shambulio la hivi karibuni la silaha dhidi ya Donald Trump, Rais wa zamani wa Marekani.

Amir Saeid Iravani, mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa 

 

Kan'ani amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeazimia kumfungulia mashtaka Trump kutokana na kuhusika kwake moja kwa moja katika mauaji ya Jenerali Qassem Soleimani, kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, lakini inakanusha kuhusika kwa namna yoyote ile na shambulio la hivi karibuni la silaha dhidi ya Trump au tuhuma kuhusu nia ya Iran na inachukulia madai hayo kuwa yana malengo na matashi ya kisiasa.

Kwa hakika, Marekani ambayo imekabiliwa na ongezeko la vurugu za kisiasa katika miaka ya hivi karibuni, badala ya kushughulikia chimbuko na sababu za ndani za kutokea kwa ghasia hizi, likiwemo jaribio la kumuua Trump katika tukio la kumpiga risasi huko Butler, Pennsylvania, kwa mara nyingine tena imejaribu kutafuta sababu za nje na katika hili imeamua kuituhumu Iran kwamba, eti imehusika na tukio hili.

Hii ni katika hali ambayo, tukio la kumpiga risasi Trump linaweza kutathminiwa kama ishara nyingine ya kuongezeka kila siku ghasia za kisiasa nchini Marekani katika miaka ya hivi karibuni, hasa baada ya kushambuliwa Bunge la Congress ya Marekani na wafuasi wa Donald Trump Januari tarehe 6, 2021.

Uchunguzi wa historia ya Marekani unaonyesha wazi kuwa viongozi wa kisiasa na wanaharakati wa kisiasa na kijamii wa nchi hiyo daima wamekuwa wakilengwa na ghasia za kisiasa na mauaji ya kigaidi. Mfano wa wazi wa suala hili ni mauaji ya kigaidi yaliyofanywa dhidi ya Rais John F. Kennedy wa Marekani, huko Dallas, Texas, Novemba 1963, mauaji ya Robert Kennedy, mgombea wa chama cha Democratic katika uchaguzi wa rais wa Marekani, Juni 1968 mjini Los Angeles, California na mauaji ya Martin Luther King, kiongozi wa harakati ya haki za kiraia mwenye asili ya Kiafrika huko Memphis, Tennessee mnamo Aprili 1968.

Hivyo, katika nchi ambayo rais, mgombea wa urais na viongozi wengine wa mapambano ya kiraia wameuawa kigaidi, jaribio la kutaka kumuua Donald Trump sio tukio la kushangaza.

Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran akihojiwa na kanali ya CNN ya Marekani

 

Kwa upande mwingine, jamii ya Marekani, hasa baada ya tukio la mashambulizi dhidi ya Bunge la Congress mnamo Januari 2021, imekumbwa na hali inayoongezeka kila siku ya mivutano na vurugu za kisiasa, ambapo moto wa tofauti za kisiasa na kiitikadi unazidi kuwaka. Katika kampeni zao za uchaguzi, Joe Biden na Donald Trump wamekuwa wakirushiana maneno makali, huku kila mmoja akimtuhumu mwenzake kuwa anataka kuiangamiza Marekani. Hivyo katika hali kama hiyo si jambo la kushangaza kumuona mtu mwenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia akichukua hatua ya kutaka kumuua kigaidi mmoja wa wagombea wa uchaguzi ujao wa rais, tena katika jamii ambayo upatikanaji wa silaha ni rahisi kuliko upatikanaji wa vitabu, na silaha ni nyingi kuliko idadi ya wakazi wake. Ikiwa vita na mapigano ya uchaguzi yalifikia kilele katika shambulio la Bunge la Marekani mnamo 2020 baada ya kufanyika uchaguzi, sasa mwaka huu 2024, vita na mapigano yanafanyika kabla ya uchaguzi.

Nukta inayotoa mguso ni kwamba uchunguzi wa maoni uliofanywa na Reuters/Ipsos baada ya kupigwa risasi Donald Trump unaonyesha kuongezeka wasiwasi wa Wamarekani kuhusu kutokea kwa machafuko nchini humu.

Kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi huo wa maoni ni kuwa, asilimia 80 ya washiriki ambao hawakuwa na tofauti kubwa kati yao katika mfungamano wao na chama cha Republican au Democratic, walikubaliana na chaguo kwamba "nchi ya Marekani inatoka nje ya udhibiti" na wakaonyesha wasiwasi wao kuhusiana na kuongezeka kwa machafuko nchini humo ambapo wasiwasi huo ulipanda kwa 7% ikilinganishwa na matokeo ya uchunguzi kama huo wa maoni uliofanywa na Reuters/Ipsos mwezi Mei mwaka huu.

Kadhalika wana wasiwasi kwamba matokeo ya uchaguzi wa urais wa Marekani 2024 mnamo Novemba 5 huenda yakasababisha ghasia zaidi za kisiasa katika nchi hiyo inayodai kuwa imara kiusalama na kidemokrasia.