Sudan yapinga ripoti ya Umoja wa Mataifa, yasema ni ya kisiasa
(last modified Sun, 08 Sep 2024 12:03:44 GMT )
Sep 08, 2024 12:03 UTC
  • Sudan yapinga ripoti ya Umoja wa Mataifa, yasema ni ya kisiasa

Sudan imekadhibisha ripoti mpya ya Jopo Huru la Umoja wa Mataifa la Kutafuta Ukweli, ambayo inazituhumu pande zinazozozana nchini humo kwa kufanya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu ambao unaweza kuwa uhalifu wa kivita.

Katika taarifa iliyotolewa Jumamosi jioni, Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imesema ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa "inakanyaga mamlaka yake", ikisisitiza kuwa imechochewa kisiasa.

Wizara hiyo ya Sudan imekosoa mwenendo wa tume hiyo, ikiishutumu kwa kukosa taaluma na uhuru kwa kuchapisha ripoti hiyo kabla ya kuiwasilisha kwa Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa.

Juzi Ijumaa, ujumbe huru wa kimataifa wa Umoja wa Mataifa wa kutafuta ukweli nchini Sudan ulitoa wito wa kuwekwa vikwazo vya silaha kote nchini Sudan kutokana na kukithiri vitendo vya kikatili zikiwemo hujuma za kutisha za kingono.

Katika ripoti yao hiyo ya kwanza tangu Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa lilipounda jopo hilo mwaka jana 2023, wajumbe wa jopo hilo wamesisitiza kwamba pande zote mbili zinazohasimiana, yaani wanajeshi wa Jeshi la Sudan (SAF) na Vikosi vya wanamgambo vya Usaidizi wa Haraka (RSF), pamoja na washirika wao, wanahusika na mashambulizi makubwa, ya kiholela na ya moja kwa moja yaliyohusisha mashambulizi ya anga na makombora dhidi ya raia, skuli, hospitali, mitandao ya mawasiliano na miundombinu mingine muhimu ya maji na umeme ikionesha kutozingatia kabisa ulinzi wa wasio wapiganaji.

Joy Ngozi Ezeilo, mmoja wa wajumbe wa jopo hilo la wataalamu huru ameeleza kwamba, waathirika walisimulia kushambuliwa wakiwa kwenye nyumba zao na kutishiwa kifo au kuumizwa kwa ndugu au watoto wao kabla ya kubakwa na zaidi ya mtu mmoja.”