Makumi waaga dunia katika mripuko wa lori la mafuta nchini Nigeria
Makumi ya watu wamepoteza maisha baada ya lori la kubeba mafuta kuripuka baada ya kugongana na gari jingine kaskazini mwa Nigeria.
Mkuu wa Idara ya Dharura ya Jimbo la Niger (NSEMA), Abdullahi Baba Arah amesema watu 48 wamethibitishwa kuaga dunia kufuatia ajali hiyo ya jana Jumapili.
Aidha Baba Arah amenukuliwa na shirika la habari la Anadolu akisema kuwa, mifugo 50 imeaga dunia kwa kuteketea kwa moto ikiwa hai kufuatia mripuko huo.
Msemaji wa Wakala wa Dharura Nigeria, Ibrahim Husseini amesema kuwa, operesheni ya kuwasaka manusuru na kuopoa miili wa wahanga wa ajali hiyo ilikuwa ikiendelea kufikia Jumapili jioni.
Gavana wa jimbo la Niger, Mohammed Umaru Bago ameseama amesikitishwa na tukio hilo, huku akizinyooshea mkono wa pole familia zilizopoteza wapendwa wao, na kuwatakia afueni ya haraka majeruhi wa mkasa huo.
Miripuko ya malori na mabomba ya kusafirishia mafuta na gesi imekuwa ikiripotiwa mara kwa mara nchini Nigeria, taifa la Afrika magharibi lenye utajiri wa bidhaa hizo.
Aidha ajali mbaya za barabarani huripotiwa mara kwa mara nchini Nigeria, na mara nyingi husababishwa na upakiaji kupita kiasi, hali mbaya ya barabarani, na kuendesha gari kwa kasi ya juu.