Utulivu wa kiasi fulani warejea Sudan Kusini
Duru za habari zimearifu kuwa hali ya utulivu wa kiasi fulani imerejea huko Sudan Kusini kufuatia uamuzi uliochukuliwa na Umoja wa Afrika wa kutuma wanajeshi wa kulinda amani nchini humo.
Uamuzi huo wa Umoja wa Afrika umechukuliwa baada ya kuongezeka mashambulizi ya silaha huko Juba mji mkuu wa Sudan Kusini kati ya vikosi vitiifu kwa Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na vile vinavyomuunga mkono Makamu wake Riek Machar.
Makubaliano mbalimbali ya amani nchini Sudan Kusini yamekuwa yakivunjwa mara kwa mara na pande husika.
Hii ni katika hali ambayo wimbi jipya la mapigano na hali ya mchafukoge iliyoikumba Sudan Kusini vimesababisha mamia ya watu kuuliwa na maelfu ya wengine kulazimika kuyahama makazi yao. Shirika la Msamaha Duniani (Amnesty International) pia limetahadharisha kuhusu hatua ya askari wa Sudan Kusini ya kuwazuia raia wa nchi hiyo kuondoka nchini humo.
Sudan Kusini iliitenga na Sudan mwaka 2011 na miaka miwili baadaye yaani mwaka 2013, nchi hiyo ilitumbukia kwenye vita vya kuwania madaraka baada ya Rais Salva Kiir kumtuhumu makamu wake, Riek Machar kwamba alipanga njama za kumpindua.
Mgogoro wa kibinadamu huko Sudan Kusini ulichanganyika na ule wa kiuchumi na kupelekea kuporomoka thamani ya fedha ya nchi hiyo na pia kupanda vibaya gharama za maisha baada ya serikali kushindwa kudhibiti mfumuko wa bei za bidhaa.