Sep 13, 2024 03:05 UTC
  • Rais wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye
    Rais wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye

Rais wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye amesema kuwa serikali yake itafanya kila liwezekanalo kukabiliana na safari hatarishi za wahamiaji baada ya mkasa wa karibuni kuua makumi ya watu.

Rais Faye alitoa hakikiho hilo jana Alkhamisi kwenye ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa X baada ya kutembelea Mbour, ambako ajali hiyo ilitokea Jumapili, ili kutoa rambirambi zake kwa familia zilizofiwa.

Amesema: Baada ya maafa yasiyovumilika ya uhamiaji haramu ulioikumba nchi, Senegal iko katika maombolezo. Ninasimama na familia zinazoomboleza na kuthibitisha dhamira yetu ya kusambaratisha mitandao ya uhamiaji haramu inayowanyanyasa watoto wetu.

Idadi ya vifo kutokana na ajali ya boti iliyokuwa imebeba wahamiaji iliyopinduka katika ufuo wa Senegal imeongezeka hadi 40 kufuatia kugunduliwa kwa miili zaidi Jumatano. Boti hiyo ilikuwa inaelekea barani Ulaya, na watu walioshuhudia wanasema kuwa, ilikuwa na abiria zaidi ya 100.

Rais wa Senegal ameshutumu "wafanya magendo ya binadamu" ambao anasema wanawatumia vibaya vijana wa Senegal waliokata tamaa kwa kuwaahidi mustakabali mwema nje ya nchi, huku wakiwapeleka kwenye hali hatarishi.

Amesisitiza kuwa, msako dhidi ya wahusika wa magendo ya binadamu na safari hizo hatari utaimarishwa, ukihusisha polisi na jeshi, "ili kutokomeza vitendo hivyo haramu."

Pwani za Senegal hutumiwa mara kwa mara na wahamiaji wa Kiafrika wanaoelekea katika Visiwa vya Kanari vya Uhispania, ambavyo vinatumika kama moja ya maeneo makuu ya watu wanaojaribu kufika Ulaya.

Tags