Sep 15, 2024 07:27 UTC
  • Maambukizo ya ugonjwa wa Mpox yaongezeka nchini Uganda

Idadi ya wagonjwa nchini Uganda walioambukizwa aina mpya ya virusi vya Mpox imeongezeka hadi 11, huku afisa mkuu wa afya akiripoti kuwa hakuna vifo vilivyosababishwa na maradhi hayo kufikia jana Jumamosi nchini humo.

Henry Gatyanga Mwebesa, Mkurugenzi Mkuu wa Huduma za Afya katika Wizara ya Afya ya Uganda amewaambia waandishi wa habari mjini Kampala kwamba, wagonjwa wote wameambukizwa spishi aina ya clade 1b, ambayo inaaminika kuwa ni aina hatari zaidi ambayo inaweza kuenea kupitia kugusana ngozi.

Uganda iliripoti kisa cha kwanza Julai 24 wakati vipimo vya maabara vya wagonjwa wawili katika hospitali moja inayopakana na Jamhuri ya kidemkrasia ya Kongo, vilipogundua kuambukizwa homa hiyo.

Hivi karibuni, Shirika la Afya Duniani (WHO) liliitangaza Mpox kuwa "dharura ya afya ya umma" kwa mara ya pili sasa katika kipindi cha miaka miwili.

Kwa mujibu wa WHO, kanda ya Afrika hivi sasa inashuhudia ongezeko la maambukizo ya homa hiyo, huku mataifa 14 ya bara hilo yakiathirika.

Shirika la Afya Duniani limetangaza kuwa, licha ya kuwa maambukizi ya ugonjwa huo yamekuwa yakiongezeka kwa kasi, lakini vifo vinavyotokana na maradhi hayo ni vichache.

Tags