Sep 16, 2024 12:22 UTC
  • Mataifa ya Afrika Magharibi yaliyojitenga kuzindua pasipoti ya pamoja

Muungano wa Mataifa ya Sahel (AES), kambi ya kikanda ambayo ilianzishwa Septemba iliyopita na viongozi wa kijeshi wa Mali, Niger na Burkina Faso, imetangaza mpango wa kuanzisha pasipoti ya pamoja ili kuimarisha ushirikiano na usalama baina yao.

Mwenyekiti wa AES ambaye pia ni rais wa Mali Kanali Assimi Goita amesema katika hotuba ya televisheni kwamba hivi karibuni muungano huo utazindua pasipoti ya pamoja ya kibayometriki ambayo pia itawezesha uhamaji wa raia katika mataifa hayo matatu.

Ametoa kauli hiyo kuadhimisha mwaka mmoja tangu kuundwa Muungano wa Mataifa ya Sahel Septemba 16 mwaka jana.

Burkina Faso, Mali na Niger ziliunda Muungano wa Mataifa ya Sahel na kutangaza kuundwa kwa kikosi cha pamoja cha kijeshi ili kukabiliana na changamoto za usalama zinazoletwa na makundi ya kigaidi katika nchi zao. 

Mataifa hayo matatu ya Afrika Magharibi yalijiondoa katika Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS), ambayo ilikuwa imetishia kuingilia kijeshi nchini Niger kufuatia mapinduzi ya kijeshi nchini humo Julai mwaka jana.

Nchi hizo tatu, zenye jumla ya watu milioni 72, zimeathiriwa na ukosefu wa utulivu unaosababishwa na makundi ya kigaidi na waasi.

Mwezi Julai mwaka huu, viongozi wa nchi hizo tatu walifanya mkutano wao wa kwanza wa pamoja katika mji mkuu wa Niger, Niamey ambapo walitangaza kuwa nchi hizo tatu zitaunda shirikisho.