Marekani yaondoka kabisa kijeshi Niger
Jeshi la Marekani limetangaza katika taarifa kuwa mpango wa kuondoa wanajeshi wake katika ardhi ya Niger umekamilika.
Kwa mujibu wa shirika la habari la CNN, Kamandi ya Afrika ya Jeshi la Marekani imesema katika taarifa kwamba mchakato wa kuondoka majeshi ya Marekani katika ardhi ya Niger ulioanza mwezi Mei 19 mwaka huu, ulikamilika katika Kambi ya 101 ya Wanahewa huko Niamey mnamo Julai 7 na kwenye Kambi ya 201 ya Wanahewa huko Agadez mnamo Agosti 5.
Kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea Niger mwaka jana, serikali ya kijeshi ya nchi hiyo ilifutilia mbali makubaliano na Marekani ambayo yaliiruhusu nchi hiyo ya Magharibi kuwa na kambi na vikosi vya kijeshi huko Niger na kuitaka kufunga kambi zake zote katika nchi hiyo ya Kiafrika zilizokuwa na wanajeshi zaidi ya elfu moja.
Sababu muhimu zaidi ya takwa hilo ni kuwa mkataba wa Marekani na serikali ya zamani ya Niger ulikuwa wa kidhalimu uliozingatia tu maslahi ya Marekani bila kujali haki, maslahi wala matakwa ya Waniger. Moja ya sababu muhimu zilizotolewa na Marekani kwa ajili ya kutuma vikosi vya kijeshi lake huko Niger ni eti kukabiliana na waasi na magaidi katika nchi za eneo la Sahel barani Afrika. Hii ni katika hali ambayo serikali ya kijeshi ya Niger, iliuchukulia mkataba huo wa serikali ya zamani na Marekani kuwa nembo ya unyonyaji mpya na ukoloni mamboleo wa nchi hiyo dhidi ya watu wa Niger.
Ufaransa ni mkoloni mkongwe barani Afrika, hususan eneo la Sahel, lakini kutokana na mapinduzi mfululizo ya kijeshi barani humo, wakoloni wa zamani kama vile Ufaransa na wakoloni wapya kama Marekani wamebadilisha nyuso zao za ukoloni wa zamani. Mapinduzi yaliyofanyika miezi michache iliyopita nchini Niger yalikuwa hatua dhidi ya ukoloni wa Marekani. Ukweli wa mambo ni kwamba kutokana na kuelimika na kupata mwamko mpya watu wa Afrika, wameongeza mapambano na upinzani wao dhidi ya wakoloni wa Magharibi, na hili linaonyesha kuwa uwanja wa uwepo wa wakoloni barani Afrika unazidi kuwa finyu.
Kuhusiana na hili, Sabrina Singh naibu msemaji wa wizara ya ulinzi ya Marekani (Pentagon) ametangaza katika taarifa kwamba uwepo wa wanajeshi wa Marekani nchini Niger ni mdogo sana na kwamba sasa watakuwa wakilinda tu usalama katika ubalozi wa Marekani nchini humo. Moja ya visingizio visivyo na msingi vinavyotumiwa na Marekani kutuma wanajeshi wake katika pembe tofauti za dunia ni eti kupambana na ugaidi, vikiwemo vikundi vya kigaidi vya Daesh na Al-Qaeda, pamoja na ghasia za ndani ya nchi na kieneo. Hii ni katika hali ambayo viongozi wa Marekani wenyewe wamekiri mara kadhaa kuwa serikali ya nchi hiyo ndiyo ilianzisha makundi hayo ya kigaidi ili kuhalalisha uwepo wao wa kijeshi katika maeneo tofauti ya dunia. Sababu kuu za Marekani kuzitwisha nchi za Kiafrika mikataba ya kidhalimu ya kijeshi ni kwanza kumfutilia mbali hasimu wake mkongwe wa kikoloni Ufaransa, kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi, na pili ni kuhalalisha ukoloni wake mpya barani humo. Hii ndio maana, msemaji wa jeshi la Niger akasema kuwa makubaliano ya serikali ya awali ya Niger na Marekani sio tu kwamba hayakuwa ya kiadilifu, bali yalipuuza kabisa matakwa na maslahi ya watu wa Niger.
Kwa msingi huo serikali ya kijeshi ya Niger iliamuru Marekani kuwaondoa wanajeshi wake 1,000 nchini humo mnamo Aprili mwaka jana, jambo ambalo lilichukuliwa kuwa kushindwa kukubwa kwa Marekani na aibu na fedheha kubwa kwa Washington.
Kabla ya mapinduzi, Niger ilikuwa mshirika mkuu wa Marekani katika kile kilichotajwa kuwa mapambano dhidi ya waasi katika eneo la Sahel, ambayo yalisababisha vifo vya maelfu ya watu na kupelekea mamilioni ya wengine kuhama makazi yao. Kwa msingi huo Waniger wanakuchukulia kuondolewa kikamilifu jeshi la Marekani katika nchi yao kuwa ni ushindi mkubwa na mafanikio ya kuvutia katika njia ya taifa lao kujidhaminia uhuru na kujitawala, jambo ambalo linaweza kuwa mfano wa kuigwa na nchi nyingine za Afrika, ambazo ni wenyeji wa majeshi ya nchi za Magharibi, ikiwemo Marekani.