Mwanaharakati Nigeria: Kimbunga cha al-Aqsa kilianika udhaifu wa Israel
(last modified Mon, 07 Oct 2024 06:17:34 GMT )
Oct 07, 2024 06:17 UTC
  • Mwanaharakati Nigeria: Kimbunga cha al-Aqsa kilianika udhaifu wa Israel

Mwanaharakati mashuhuri wa haki za binadamu nchini Nigeria amesema Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa ya Oktoba 7, 2023 iliyofanywa na wanamapambano wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS ilifichua namna utawala haramu wa Israel ulivyo dhaifu sanjari na kuugutusha ulimwengu juu ya kadhia ya Palestina.

Katika mahojiano maalumu na shirika la habari la Iran Press katika jimbo la Gombe la kaskazini mashariki mwa Nigeria, Ibrahim Yusuf, Mkuu wa Kituo cha Kupigania Ustawi nchini Nigeria (ACD) amesema, "Athari za Kimbunga cha al-l Aqsa haziwezi kupuuzwa kwa sababu zimebadilisha simulizi (mlingano) duniani kote, na pia zimefichua jinsi utawala wa Israel ulivyo dhaifu."

Amebainisha kuwa: Kabla ya Kimbunga cha al-Aqsa, kulienezwa propaganda na habari za uwongo kwamba, Israeli ndilo dola lenye nguvu zaidi na lisiloshindika katika eneo la Mashariki ya Kati.

Yusuf ameashiria operesheni ya hivi karibuni ya kulipiza kisasi na kuutia adabu utawala wa Kizayuni iliyofanywa na Iran na kusema, "Ukitazama jinsi (Wazayuni) walivyoshambuliwa wiki iliyopita na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, asilimia tisini (au zaidi) ya makombora ya Hypersonic ya Iran yalipiga shabaha zilizokusudiwa na kuisababishia uharibifu na hasara kubwa Israel."

Wanigeria wamekuwa wakiandamana kuonyesha mshikamano na Wapalestina

Mkuu wa Kituo cha Kupigania Ustawi nchini Nigeria amesisitiza kuwa, nchi za dunia lazima zianze kujinasibisha na watu wanaodhulumiwa wa Palestina kwa misingi ya ubinadamu. "Ima uwe pamoja na madhalimu au pamoja na Wapalestina wanaodhulumiwa," ameongeza.

Mwanaharakati huyo wa haki za binadamu wa Nigeria ameeleza bayana kuwa, "Kujikurubisha wewe na nchi yako na watu wanaodhulumiwa wa Palestina ni ishara kwamba upo thabiti, kwa sababu Marekani na washirika wake wanatawala akili za watu."