Afrika Kusini: Tutafuatilia faili na mauaji ya kimbari ya Israel ICJ
Afrika Kusini imetangaza azma yake ya kufuatilia kesi ya mauaji ya halaiki iliyowasilisha dhidi ya utawala ghasibu wa Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) "licha ya mashinikizo kutoka kwa baadhi ya nchi ya kuitaka kuondoa kesi hiyo.
Hayo yameelezwa na Zane Dangor, Katibu Mkuu wa Kitendo cha Mahusiano ya Kimataifa ya Afrika Kusini ambaye amesisitiza kuwa, taifa hilo limeazimia kwa dhati kuendelea na machakato wake wa kufuatilia kesi ya mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya Palestina iliyoiwasilisha katika Mahakama ya Kiamataifa ya Haki (ICJ) na kwamba, mashinikizo dhidi yake hayawezi kuwa na taathira katika kadhia hiyo.
Dangor amedokeza kuwa wamekamilisha hatua ya maandalizi ya ombi ambalo watawasilisha katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki mnamo Oktoba 28 ili kuendeleza kesi hiyo.
Hivi majuzi pia Ofisi ya Rais wa Afrika Kusini ilitangaza katika taarifa yake kwamba, itaendelea kufuatilia kesi ya mauaji ya halaiki ya utawala wa Kizayuni katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) hadi hukumu yake itakapotolewa.
Tarehe 29 Disemba 2023, Afrika Kusini iliwasilisha malalamiko dhidi ya utawala wa Kizayuni kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kwa madai ya kukiuka Makubaliano ya Kuzuia Mauaji ya Kimbari, ambayo yalipitishwa mwaka 1948.
Mmahakama hiyo kuu ya Umoja wa Mataifa ilitoa maamuzi matatu ya muda mnamo Januari 26, Machi 28 na Mei 24.
ICJ iliiamuru Israel kuchukua hatua zote ndani ya uwezo wake kuzuia mauaji ya kimbari huko Gaza, kuruhusu upatikanaji wa chakula bila vikwazo katika eneo la Palestina lililozingirwa, na kusitisha mara moja uvamizi wake wa kijeshi katika mji wa kusini wa Rafah. Israel imepuuza maagizo hayo yote ya ICJ.