UN yapitisha muswada wa kuangamizwa silaha za kemikali za Libya
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha kwa kauli moja muswada wa kuhamishia silaha za kemikali za Libya nje ya nchi hiyo kwa ajili ya kuharibiwa.
Muswada wa azimio hilo la Umoja wa Mataifa la kusimamia shughuli ya kuhamisha silaha hizo kutoka Libya kwenda nje ya nchi kwa minajili ya kuziangamiza, ulipendekezwa na Uingereza. Kazi hiyo itasimamiwa na sekretarieti ya Umoja Mataifa na nchi wanachama wa mkataba wa kuzuia uenezaji na utumiaji wa silaha za kemikali. Azimio hilo limepitishwa kufuatia ombi la serikali ya Libya la kuharibiwa silaha hizo.
Kadhalika azimio hilo limeitahadharisha jamii ya kimataifa juu ya hatari ya silaha hilo kuingia mikononi mwa makundi ya kufurutu ada na ya kigaidi.
Libya ilijiunga na mkataba wa kuzuia kueneza silaha za kemikali mwaka 2004.