Chama tawala cha Zimbabwe chatoa wito wa kufutwa majina ya kikoloni nchini humo
(last modified Thu, 31 Oct 2024 11:11:23 GMT )
Oct 31, 2024 11:11 UTC
  • Chama tawala cha Zimbabwe chatoa wito wa kufutwa majina ya kikoloni nchini humo

Majina ya majimbo na maeneo nchini Zimbabwe ambayo yanahusishwa na historia ya ukoloni wa nchi hiyo yanapaswa kubadilishwa.

Wito huu umetolewa na Patrick Chinamasa, Katibu wa Masuala ya Kisheria wa chama tawala cha Zanu-PF cha Zimbabwe, wakati wa Mkutano wa 21 wa Mwaka wa Kitaifa wa Zanu-PF.

Chinamasa amesema: "Katika urithi wa vita vya ukombozi, chama kinaielekeza serikali kuharakisha kubadilisha na kuondoa majina ya kikoloni, ambayo yanagawanya taifa."

Kwa miaka mingi, kumekuwa na miito ya kubadili jina la kivutio mashuhuri cha utalii duniani cha Zimbabwe, Victoria Falls au Maporomoko ya Victoria kwani kubakia jina hili ni sawa na kuendelea kuheshimu urithi wa ukoloni na Malkia Victoria, ambaye maporomoko hayo yamepewa jina lake.

Wanaharakati wanasema kuwa haina maana kuendelea kuwa na majina ya kikoloni na badala yake yanafaa kubadilishwa na ya kienyeji.

Wazimbabwe wanasisitiza kuwa David Livingstone hakuwa mtu wa kwanza kuona maporomoko ya maji ya Victoria, na hivyo ni lazima maporomoko hayo yabadilishwe na yarejee katika jina lake la asili ambalo ni Mosi-Oa-Tunya.

Maporomoko ya maji ya Victoria yalipewa jina la mfalme wa Uingereza, Malkia Victoria na mmishonari, David Livingstone, ambaye alikuwa mzungu wa kwanza kuona mojawapo ya maajabu saba ya kimaumbile duniani.

Kabla ya uhuru kutoka kwa Uingereza mwaka 1980, Zimbabwe iliitwa Rhodesia, kutokana na jina la gavana wa kikoloni, Rhodes.