Takriban watu 321 wameshafariki dunia katika mafuriko nchini Nigeria
Takriban watu 321 wamepoteza maisha na wengine zaidi ya 740,000 wamelazimika kuhama makazi yao nchini Nigeria tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi hivi sasa kutokana na mafuriko yaliyokumba maeneo mengi ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Chukwuma Soludo, Mkuu wa Mkoa wa Anambra wa kusini mashariki mwa Nigeria amewaambia waandishi wa habari mjini Abuja baada ya kufanyika kikao cha Baraza la Taifa la Uchumi lililoongozwa na Makamu wa Rais Kashim Shettima kwamba, watu wapatano 2,854 wameshajeruhiwa katika mafuriko hayo ambayo zaidi yamesababishwa na mvua za muda mrefu katika nchi hiyo yenye watu wengi zaidi barani Afrika.
Amesemaa: "Nchi yetu imekumbwa na hali ya dharura ya kitaifa kutokana na mafuriko na ripoti zinasema kuwa, hili ni janga kubwa la kitaifa, kwani mvua zimesababisha watu wengi kuhama makazi yao na kupoteza maisha na yameharibu mashamba na makazi ya watu wengi."
Mkuu wa Mkoa huyo ameongeza kuwa, mikoa 34 kati ya 36 ya Nigeria imekumbwa na mafuriko na maeneo 217 kati ya 774 ya serikali za mitaa yameathiriwa. Mafuriko hayo yamesababisha watu wasiopungua 740,743 kuhama makazi yao na yameharibu au kuathiri nyumba 281,000 na mashamba 258,000 yaliyokuwa na mazao ya kilimo.
Baraza la Taifa la Uchumi ambalo kisheria linaongozwa na Makamu wa Rais na linajumuisha pia wakuu wa mikoa yote 36 ya Nigeria, limetoa amri ya kufanyika uchunguzi wa kina wa kiuadilifu ili kubaini hali ya njia za maji na mabwawa kwa shabaha ya kupunguza athari mbaya ya mafuriko.