Mke wa zamani wa Laurent Gbagbo kugombea urais Ivory Coast
Orodha ya wagombea wa urais nchini Ivory Coast imezidi kuwa kubwa. Mgombea aliyejitokeza hivi karibuni zaidi ni mke wa zamani wa Rais wa zamani wa nchi hiyo, Laurent Gbagbo.
Simone Ehivet ameshinda kwenye mchujo wa chama chake cha Movement of Capable Generations (MGC) katika kikao kikuu cha chama kilichofanyika kwenye mji wake wa asili wa Moossou wa kusini mashariki mwa Ivory Coast.
Katika hotuba iliyokuwa na mvuto maalumu, Ehivet alitangaza vipaumbele vyake ikiwa ni pamoja na kujenga mshikamano wa kitaifa kupitia kushajiisha watu kusameheana pamoja na usalama wa chakula na ustawi wa viwanda.
Laurent Gbagbo na Simone walitalikiana mwezi Juni 2023 baada ya miaka 34 ya ndoa na miongo kadhaa ya harakati za pamoja.
Kitaaluma Ehivet ni mwalimu na alianza uanaharakati kama mwanaharakati wa vyama vya wafanyakazi katika miaka ya 1970. Nyota yake ya kisiasa iling'ara alipokutana na Gbagbo mwaka 1973.
Kwa pamoja, walianzisha chama cha Popular Ivorian Front mwaka 1982 kwa shabaha ya kuchochea upinzani dhidi ya utawala wa Felix Houphouet Boigny.
Wakati Gbagbo alipotiwa mbaroni na kufungwa jela, nafasi yake ilichukuliwa na Pascal Affi N'Guessan ambaye pia ametangaza kugombea katika uchaguzi wa 2025.