Waandamanaji washambulia ubalozi wa Marekani Kinshasa, waliouawa Goma wapindukia mia moja
(last modified Wed, 29 Jan 2025 07:21:32 GMT )
Jan 29, 2025 07:21 UTC

Sambamba na machafuko yanayoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), raia wa nchi hiyo wameshambulia ubalozi wa Marekani na nchi nyingine kadhaa za Magharibi mjini Kinshasa na kuchoma moto baadhi ya ofisa za balozi hizo wakipinga uingiliaji kati wa nchi hizo katika masuala ya ndani ya nchi hiyo.

Raia wanaoandamana katika mji mkuu wa Congo wanaishutumu Washington kuwa inawaunga mkono waasi wanaojulikana kwa jina la M23, ambao wanadai wameuteka mji muhimu wa Goma mashariki mwa nchi hiyo.

Waandamanaji hao walikusanyika mbele ya ubalozi wa Marekani katika mji mkuu wa Congo, wakipiga nara kama vile "kifo kwa mabeberu" na "Wezi, ondokeni Congo." Vilevile walichoma moto matairi mbele ya ubalozi huo ambao umeteketeza sehemu ya kuta zake na nyumba ya mlinzi. 

Congo DR

Balozi za Ufaransa, Uholanzi, Ubelgiji, Rwanda, Uganda, na Kenya pia zimeshambuliwa na waandamanaji waliokuwa na hasira katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Wakati huo huo, inaripotiwa kuwa watu wasiopungua 100 wameuawa na zaidi ya 1,000 kujeruhiwa, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na hospitali kadhaa za Goma.

Ripoti zinasema hospitali za Goma zimezidiwa na idadi kubwa ya majeruhi na kwamba miili imetapakaa huku na kule katika mitaa ya mji huo.

Jumatatu iliyopita, waasi wa M23 ambao Umoja wa Mataifa unasema wanaungwa mkono na Rwanda, waliingia mjini Goma na kudai kuwa wameuteka na kuudhibiti mji huo muhimu wa mashariki wa Congo DR. 

Maelfu ya raia wa Goma wamelazimika kuwa wakimbizi kutokana na mapigano yanayoendelea katika mji huo. 

Mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuhusu hali ya machafuko mashariki mwa DRC, unatarajiwa kufanyika leo Jumatano, Januari 29 kujadili kadhia hiyo.