Sudan yaafiki kuanzishwa nchini humo kambi ya jeshi la wanamaji la Russia
(last modified Thu, 13 Feb 2025 02:52:06 GMT )
Feb 13, 2025 02:52 UTC
  • Sudan yaafiki kuanzishwa nchini humo kambi ya jeshi la wanamaji la Russia

Khartoum na Moscow zimekubaliana juu ya kuanzishwa kituo cha jeshi la wanamaji la Russia nchini Sudan.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan, Ali Youssef Ahmed Al-Sharif katika mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na mwenzake wa Russia, Sergey Lavrov huko Moscow jana Jumatano.

Al-Sharif amethibitisha kwamba, majadiliano yamekamilika kwa mafanikio, akieleza kuwa, "Kwa hivyo, jambo hilo ni rahisi sana. Sina cha kuongeza. Tumekubaliana katika kila jambo.”

Kwa mujibu wa shirika la habari la TASS, makubaliano hayo, ambayo yaliibuka kwa mara ya kwanza mnamo Disemba mwaka 2020, yanaelezea kwa kina juu ya kuanzishwa kituo cha msaada wa kilojistiki cha Jeshi la Wanamaji la Russia huko Sudan.

Kambi hiyo itatumika kama kitovu cha ukarabati na usambazaji wa meli. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, wafanyakazi wa kituo hicho hawatazidi 300, na meli nne za Russia, hicho kikiwa kiwango cha juu zaidi, zitaruhusiwa kutia nanga katika kituo hicho kwa wakati mmoja.

Kufuatia mazungumzo hayo, Lavrov amesisitiza tena "msimamo wa Russia juu ya haja ya kusitishwa kwa haraka kwa uhasama na kuanzishwa kwa mazungumzo jumuishi ya kitaifa" ya kutafutia ufumbuzi mzozo wa Sudan kati ya Jeshi la serikali (SAF) na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF), bila kuingiliwa na maajinabi.

Mzozo huo wa kikatili umepelekea kuuawa makumi ya maelfu ya watu tangu Aprili mwaka 2023, mbali na kusababisha mamilioni ya Wasudan kuyahama makazi yao.