Viongozi wa kanisa Kongo wakutana na waasi wa M23
Ujumbe wa taasisi mbili za kanisa nchini Jamhuri wa Kidemokrasi ya Kongo umekutana na waasi wa M23 mashariki mwa taifa hilo katika juhudi za hivi karibuni za kusaka amani na mazungumzo baada ya wiki kadhaa za mapigano.
Ujumbe huo wa pamoja kutoka Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini Kongo na ule wa Kanisa la Kristo la Kongo uliwasili Goma siku ya Jumatano na kukutana na kiongozi wa kisiasa wa kundi la M23, Corneille Nangaa.
Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu la Kongo, Askofu Donatien Nshole, amesema mkutano na M23 ulikuwa nafasi ya kutafuta njia za kumaliza vita haraka iwezekanavyo. Amesema taasisi hizo mbili kubwa za kidini zinaamini mzozo unaoendelea nchini humo hautamalizwa kwa njia za kijeshi.
Mkutano huo umefanyika wakati inaarifiwa waasi hao wanaoungwa mkono na Rwanda wanaendelea na mapigano wakisonga mbele kuelekea mji mkuu wa jimbo la Kivu Kusini wa Bukavu. Ujumbe wa makanisa ya Kikatoliki na Kiprotestanti umetoa wito wa kusitishwa mapigano mjini Goma wakati wa ziara ya viongozi wa waasi waliouteka mji huo mashariki mwa DRC. Askofu wa Kanisa Katoliki Donatien Nshole amesema makanisa yote mawili yameanza juhudi za upatanishi kati ya waasi na serikali.
"Ziara yetu inalenga kuhimiza mazungumzo, kusikiliza wasiwasi, na kuongeza ufahamu juu ya haja ya haraka ya suluhisho la amani kumaliza mgogoro," alisema. "Tunaamini kwamba AFC/M23 inaweza kuchukua jukumu muhimu katika mchakato huu wa kujenga amani," aliongeza.