OCHA: Mamilioni ya watu wameendelea kutoroka makazi yao nchini DRC
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema kuwa, mamilioni ya watu wanaendelea kuyahama makazi yao Kivu Kaskazini na Kivu Kusini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Huko Kivu Kaskazini inaripotiwa kuwa watu 110,000 wameondoka katika kambi za wakimbizi huko Goma na kuanza kuhamia katika vijiji vya Masisi, Rutshuru na Nyiragongo.
OCHA na washirika wake wa msuala ya kibinadamu pia wana wasiwasi kuhusu uporaji unaoendelea wa miundombinu katika kambi za wakimbizi wa ndani.
Hali hii inasababisha kuporwa kwa vifaa vya misaada ya kibinadamu katika maeneo hayo, ikiwa ni pamoja na usambazaji wa maji, vituo vya afya, na vituo vya matibabu ya kipindupindu, na kusababisha hasara kubwa ya kifedha na kupunguza uwezo wa kukabiliana na idadi kubwa ya watu waliopoteza makazi yao.
M23 ambalo ni kundi maarufu zaidi kati ya zaidi ya makundi 100 ya wanamgambo wenye silaha wanaopigania kudhibiti eneo la mashariki mwanchi hiyo lenye utajiri wa madini, mwishoni mwa Januari liliteka Goma, mji mkubwa zaidi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kusonga mbele katika mji wa Goma kundi la M23 kumesababisha vifo vya watu wasiopungua 2,000 katika viunga vya mji huo.
Ingawa waasi wa M23 walitangaza kusitisha mapigano kwa upande mmoja wiki iliyopita, hata hivyo wenyeji wanaendelea kuripoti kujiri mapigano kati ya M23 na vikosi vya serikali ya Kongo.
Hivi karibuni wakuu wa nchi wanachama katika jumuiya mbili za kikanda za Mashariki na Kusini mwa Afrika walifanya mkutano wa aina yake katika mji mkuu wa kibiashara Tanzania, Dar es Salaam wakijaribu kutafuta suluhisho la kumaliza mgogoro wa mashariki mwa Kongo DR.